Translations | Suras |
KISWAHILI | |
15 - AL - HIJR | |
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU. | |
1 | Alif Lam Ra. (A.L.R). Hizi ni Aya za Kitabu na Qur'ani inayo bainisha. |
2 | HUENDA ikawa walio kufuru wakatamani wange kuwa Waislamu. |
3 | Waache wale, na wastarehe, na iwazuge tamaa. Watakuja jua. |
4 | Na hatukuuangamiza mji wowote ule ila ulikuwa na muda wake maalumu. |
5 | Hawawezi watu wowote kuitangulia ajali yao, wala kuchelewa. |
6 | Na walisema: Ewe uliyeteremshiwa Ukumbusho! Hakika wewe ni mwendawazimu. |
7 | Mbona hutuletei Malaika ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli? |
8 | Sisi hatuwateremshi Malaika ila kwa sababu ya haki, na hapo hawatapewa muhula. |
9 | Hakika Sisi ndio tulio teremsha Ukumbusho huu, na hakika Sisi ndio tutao ulinda. |
10 | Na hakika tulikwisha watumia Mitume mataifa ya mwanzo. |
11 | Na hakuwafikia Mtume ila walimkejeli. |
12 | Na kama hivi ndivyo tunavyo ingiza katika nyoyo za wakosefu. |
13 | Hawayaamini haya, na hali ya kuwa umekwisha wapitia mfano wa watu wa kale. |
14 | Na lau tungeli wafungulia mlango wa mbingu, wakawa wanapanda, |
15 | Basi wangeli sema: Macho yetu yamelevywa, bali sisi wenyewe tumerogwa. |
16 | Na hakika tumeweka katika mbingu vituo vya sayari, na tumezipamba kwa wenye kuangalia. |
17 | Na tumezilinda na kila shetani afukuzwaye. |
18 | Isipo kuwa mwenye kusikiliza kwa kuibia, naye hufuatwa na kijinga cha moto kinacho onekana. |
19 | Na ardhi tumeitandaza na humo tumeweka milima, na tumeotesha kila kitu kwa kiasi chake. |
20 | Na tumekujaalieni humo vitu vya maisha yenu, na ya hao ambao nyinyi sio wenye kuwaruzuku. |
21 | Na hakuna chochote ila asili yake inatokana na Sisi; wala hatukiteremshi ila kwa kipimo maalumu. |
22 | Na tunazipeleka pepo za kupandishia, na tunateremsha kutoka mbinguni maji, kisha tukakunywesheni maji hayo. Wala si nyinyi mnayo yaweka. |
23 | Na Sisi ndio tunao huisha na tunao fisha. Na Sisi ndio Warithi. |
24 | Na tunawajua walio tangulia katika nyinyi, na tunawajua walio taakhari. |
25 | Na hakika Mola wako Mlezi ndiye atakaye wakusanya. Hakika Yeye ni Mwenye hikima na Mjuzi. |
26 | Na tulimuumba mtu kwa udongo unao toa sauti, unao tokana na matope yaliyo tiwa sura. |
27 | Na majini tuliwaumba kabla kwa moto wa upepo umoto. |
28 | Na Mola wako Mlezi alipo waambia Malaika: Hakika Mimi nitamuumba mtu kwa udongo unao toa sauti, unao tokana na matope yaliyo tiwa sura. |
29 | Basi nitakapo mkamilisha na nikampulizia roho yangu, basi mumwangukie kumsujudia. |
30 | Basi Malaika wote pamoja walimsujudia, |
31 | Isipo kuwa Iblisi. Yeye alikataa kuwa pamoja na walio sujudu. |
32 | (Mwenyezi Mungu) akasema: Ewe Iblisi! Una nini hata hukuwa pamoja na walio sujudu? |
33 | Akasema: Haiwi mimi nimsujudie mtu uliye muumba kwa udongo unao toa sauti, unao tokana na matope yenye sura. |
34 | (Mwenyezi Mungu) akasema: Basi toka humo, kwani hakika wewe ni maluuni! |
35 | Na hakika juu yako ipo laana mpaka Siku ya Malipo. |
36 | Akasema (Iblisi): Mola wangu Mlezi! Nipe muhula mpaka siku watapo fufuliwa. |
37 | (Mwenyezi Mungu) akasema: Hakika wewe ni katika walio pewa muhula |
38 | Mpaka siku ya wakati maalumu. |
39 | Akasema: Mola wangu Mlezi! Ilivyo kuwa umenitia makosani, basi nahakikisha nitawazaini hapa duniani na nitawapoteza wote, |
40 | Ila waja wako walio safika. |
41 | Akasema: Hii Njia ya kujia kwangu Iliyo Nyooka. |
42 | Hakika waja wangu, wewe hutakuwa na mamlaka juu yao, isipo kuwa wale wapotofu walio kufuata. |
43 | Na bila shaka Jahannamu ndipo pahali pao walipo ahidiwa wote. |
44 | Ina milango saba; na kwa kila mlango iko sehemu walio tengewa. |
45 | Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na chemchem. |
46 | (Wataambiwa:) Ingieni kwa salama na amani. |
47 | Na tutaondoa chuki iliyo kuwamo vifuani mwao, wawe ndugu juu ya viti vya enzi wameelekeana. |
48 | Humo hayatawagusa machofu, wala hawatatolewa humo. |
49 | Waambie waja wangu ya kwamba Mimi ndiye Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. |
50 | Na kwamba adhabu yangu ndio adhabu iliyo chungu! |
51 | Na uwape khabari za wageni wa Ibrahim. |
52 | Walipo ingia kwake na wakasema: Salama! Yeye akasema: Hakika sisi tunakuogopeni. |
53 | Wakasema: Usiogope. Sisi tunakubashiria kijana mwenye ujuzi. |
54 | Akasema: Mnanibashiria nami uzee umenishika! Basi kwa njia gani mnanibashiria? |
55 | Wakasema: Tunakubashiria kwa haki; basi usiwe miongoni mwa wanao kata tamaa. |
56 | Akasema: Na nani anaye kata tamaa na rehema ya Mola wake Mlezi ila wale walio potea? |
57 | Akasema: Hebu nini amri yenu, enyi wajumbe? |
58 | Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwa kaumu ya wakosefu! |
59 | Isipo kuwa walio mfuata Luut'i. Bila ya shaka sisi tutawaokoa hao wote. |
60 | Ila mkewe. Tunakadiria huyo atakuwa miongoni watao bakia nyuma. |
61 | Basi wale wajumbe walipo fika kwa Luut'i, |
62 | Alisema (Luut'i): Hakika nyinyi ni watu msio juulikana. |
63 | Wakasema: Bali sisi tumekuletea yale waliyo kuwa wakiyafanyia shaka. |
64 | Na tumefika kwako kwa Haki, na hakika sisi tunasema kweli. |
65 | Basi ondoka na ahli zako usiku ungalipo, nawe ufuate nyuma yao, wala yeyote kati yenu asigeuke nyuma. Na mwende mnapo amrishwa. |
66 | Na tukamfunulia hukumu hiyo, ya kwamba hata wa mwisho wao hao ikifika asubuhi atakuwa kesha katiliwa mbali. |
67 | Na wakaja watu wa mji ule nao furahani. |
68 | Akasema: Hakika hawa wageni wangu, basi msinifedheheshe. |
69 | Na mcheni Mwenyezi Mungu, wala msinihizi. |
70 | Wakasema: Sisi hatukukukataza usimkaribishe yeyote? |
71 | Akasema: Hawa binti zangu, ikiwa nyinyi ni watendaji. |
72 | Naapa kwa umri wako! Hakika hao walikuwa katika ulevi wao, wakihangaika ovyo. |
73 | Ukelele ukawatwaa wakipambaukiwa. |
74 | Na tukaigeuza nchi juu chini, na tukawanyeshea mvua ya mawe ya udongo wa Motoni. |
75 | Hakika katika hayo zipo ishara kwa waaguzi. |
76 | Na miji hii ipo kwenye njia inayo pitiwa. |
77 | Hakika katika hayo ipo ishara kwa Waumini. |
78 | Na hakika watu wa Kichakani walikuwa wenye kudhulumu. |
79 | Kwa hivyo tukawaadhibu. Na nchi mbili hizi ziko kwenye njia ilio wazi. |
80 | Na bila ya shaka wakaazi wa Hijr waliwakanusha Mitume. |
81 | Na tuliwapa ishara zetu, nao wakazipuuza. |
82 | Nao walikuwa wakichonga majumba katika milima kwa amani. |
83 | Basi ukelele ukawatwaa asubuhi. |
84 | Hayakuwafaa waliyo kuwa wakiyachuma. |
85 | Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake ila kwa ajili ya Haki. Na hakika Kiyama kitafika. Basi samehe msamaha mzuri. |
86 | Hakika Mola wako Mlezi ndiye Muumbaji Mjuzi. |
87 | Na tumekupa Aya saba zinazo somwa mara kwa mara, na Qur'ani Tukufu. |
88 | Usivitumbulie macho yako vitu tulivyo waneemesha makundi fulani kati yao, wala usiwahuzunikie. Na wainamishie bawa lako (la huruma) Waumini. |
89 | Na sema: Hakika mimi ni mwonyaji mwenye kubainisha. |
90 | Kama hivyo tuliwateremshia walio gawa, |
91 | Ambao wakaifanya Qur'ani vipande vipande. |
92 | Basi Naapa kwa Mola wako Mlezi! Tutawahoji wote, |
93 | Kwa waliyo kuwa wakiyatenda. |
94 | Basi wewe yatangaze uliyo amrishwa, na jitenge na washirikina. |
95 | Hakika Sisi tunatosha kukukinga na wanao kejeli. |
96 | Hao wanao fanya kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu yupo mungu mwingine. Basi, watakuja jua! |
97 | Na Sisi tunajua kwa hakika kuwa wewe kifua chako kinaona dhiki kwa hayo wayasemayo. |
98 | Basi mtakase Mola wako Mlezi kwa kumhimidi, na uwe miongoni wanao msujudia. |
99 | Na muabudu Mola wako Mlezi mpaka ikufikie Yakini. |
ReadTheQuran.org |