Translations Suras
KISWAHILI

18 - AL - KAHF

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.

 
1Kuhimidiwa ni kwa Mwenyezi Mungu, ambaye amemteremshia mja wake Kitabu, wala hakukifanya kina upogo.
 
2Kimenyooka sawa, ili kitoe onyo kali kutoka kwake, na kiwabashirie Waumini watendao mema kwamba watapata ujira mzuri.
 
3Wakae humo milele.
 
4Na kiwaonye wanao nena: Mwenyezi Mungu ana mwana.
 
5Wao hawana ujuzi wa jambo hili, wala baba zao. Ni neno kuu hilo litokalo vinywani mwao. Hawasemi ila uwongo tu.
 
6Huenda ukajihiliki nafsi yako kwa ajili yao, kuwasikitikia kwa kuwa hawayaamini mazungumzo haya!
 
7Kwa hakika tumevifanya vilioko juu ya ardhi kuwa ni pambo lake ili tuwafanyie mtihani, ni nani kati yao wenye vitendo vizuri zaidi.
 
8Na hakika Sisi tutavifanya vyote vilio juu ya ardhi kuwa kama nchi ilio pigwa na ukame.
 
9Bali unadhani ya kwamba wale Watu wa Pangoni na Maandishi walikuwa ni ajabu miongoni mwa ishara zetu?
 
10Vijana hao walipo kimbilia kwenye pango walisema: Mola wetu Mlezi! Tupe rehema itokayo kwako, na tutengezee uwongofu katika jambo letu.
 
11Tukayaziba masikio yao kuwalaza humo pangoni kwa muda wa miaka kadhaa wa kadhaa.
 
12Kisha tukawazindua ili tujue ni lipi katika makundi mawili lilio hisabu sawa muda walio kaa.
 
13Sisi tunakusimulia khabari zao kwa kweli. Hakika wao walikuwa ni vijana walio muamini Mola wao Mlezi. Na Sisi tukawazidisha uwongofu.
 
14Na tukazitia nguvu nyoyo zao walipo simama na wakasema: Mola wetu Mlezi ni Mola Mlezi wa mbingu na ardhi. Hatutamwita mwenginewe kabisa badala yake kuwa ni Mungu. Hivyo itakuwa tumesema jambo la kuvuka mpaka.
 
15Hawa watu wetu wameshika miungu mingine badala yake Yeye. Kwa nini basi hawawatolei uthibitisho ulio dhaahiri? Na nani aliye dhaalimu zaidi kuliko anaye mzulia uwongo Mwenyezi Mungu?
 
16Na mkijitenga nao na vile wanavyo viabudu badala ya Mwenyezi Mungu, basi kimbilieni pangoni, akufungulieni Mola wenu Mlezi rehema yake, na akutengenezeeni ya kukufaeni katika mambo yenu.
 
17Na unaliona jua linapo chomoza linainamia kuliani mwao kutoka hapo pangoni; na linapo kuchwa linawakwepa kushotoni, na wao wamo katika uwazi wa pango. Hizo ni katika ishara za Mwenyezi Mungu. Ambaye Mwenyezi Mungu anamwongoa basi huyo ni mwenye kuongoka. Na anaye muacha kupotea basi hutampatia mlinzi wala mwongozi.
 
18Nawe utawadhania wamacho, na hali wamelala. Nasi tunawageuza kulia na kushoto. Na mbwa wao amenyoosha miguu yake ya mbele kizingitini. Kama ungeli watokea hapana shaka ungeli geuka kuwakimbia, nawe umejaa khofu.
 
19Na kwa namna hii tuliwainua usingizini wapate kuulizana wao kwa wao. Alisema msemaji katika wao: Mmekaa muda gani? Wakasema: Tumekaa siku moja au sehemu ya siku. Wakasema: Mola wenu Mlezi anajua zaidi muda mlio kaa. Hebu mtumeni mmoja wenu na hizi fedha zenu ende mjini, akatazame chakula chake kipi kilicho bora kabisa akuleteeni cha kukila. Naye afanye mambo hayo kwa busara, wala asikutajeni kabisa kwa yeyote.
 
20Kwani wao wakikutambueni watakupigeni mawe, au watakurudisheni katika dini yao; na hapo hamtafanikiwa kabisa!
 
21Na namna hivi tuliwa juulisha kwa watu wapate kujua ya kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli, na kwamba Saa haina shaka. Walipo kuwa wakigombania jambo lao wao kwa wao walisema: Jengeni jengo juu yao. Mola wao Mlezi anawajua vyema. Wakasema walio shinda katika shauri yao: Bila ya shaka tutawajengea msikiti juu yao.
 
22Watasema: Walikuwa watatu, wa nne wao ni mbwa wao. Na wanasema: Walikuwa watano, wa sita wao ni mbwa wao. Wanavurumisha ovyo. Na wanasema: Walikuwa saba, na wa nane wao ni mbwa wao. Sema: Mola wangu Mlezi ndiye anaye jua sawa sawa hisabu yao. Hawawajui ila wachache tu. Basi usibishane juu yao ila kwa mabishano ya juu juu tu hivi. Wala usiulize khabari zao kwa yeyote yule.
 
23Wala usisema kamwe kwa jambo lolote lile: Hakika nitalifanya hilo kesho -
 
24Isipo kuwa Mwenyezi Mungu akipenda. Na mkumbuke Mola wako Mlezi pale unapo sahau, na sema: Asaa Mola wangu Mlezi ataniongoa kwenye uwongozi ulio karibu zaidi kuliko huu.
 
25Na walikaa katika pango lao miaka mia tatu, na wakazidisha tisa.
 
26Sema: Mwenyezi Mungu anajua zaidi muda walio kaa. Ni zake tu siri za mbingu na ardhi. Kuona kulioje na kusikia kwake! Hawana mlinzi isipo kuwa Yeye, wala hamshirikishi yeyote katika hukumu yake.
 
27Na soma uliyo funuliwa katika Kitabu cha Mola wako Mlezi. Hapana wa kubadilisha maneno yake. Wala nawe hutapata makimbilio isipo kuwa kwake.
 
28Na isubirishe nafsi yako pamoja na wanao muomba Mola wao Mlezi asubuhi na jioni, hali ya kuwa wanataka radhi yake. Wala macho yako yasiwaruke kwa kutaka pambo la maisha ya dunia. Wala usimt'ii tuliye mghafilisha moyo wake asitukumbuke, na akafuata matamanio yake yakawa yamepita mpaka.
 
29Na sema: Hii ni kweli itokayo kwa Mola wako Mlezi. Basi atakaye, aamini. Na atakaye, akatae. Hakika Sisi tumewaandalia wenye kudhulumu Moto ambao utawazunguka kama khema. Na wakiomba msaada watasaidiwa kwa kupewa maji kama mafuta yaliyo tibuka. Yatayo wababua nyuso zao. Kinywaji hicho ni kiovu mno! Na matandiko hayo ya kupumzikia ni maovu mno!
 
30Hakika wale walio amini na wakatenda mema - hakika Sisi hatupotezi ujira wa anaye tenda mema.
 
31Hao watapata Bustani za milele, zinazo pita mito kati yake. Humo watapambwa kwa mavazi ya mikononi ya dhahabu, na watavaa nguo za kijani za hariri na at'ilasi, huku wakiegemea humo juu ya makochi. Ni malipo bora hayo! Na matandiko mazuri mno ya kupumzikia!
 
32Na wapigie mfano wa watu wawili: mmoja wao tulimpa vitalu viwili vya mizabibu, na tukavizungushia mitende, na kati yake tukatia mimea ya nafaka.
 
33Na hivyo vitalu viwili vikitoa mazao yake, wala hapana kitu katika hayo kilicho tindikia. Na ndani yake tukapasua mito.
 
34Naye alikuwa na mazao mengi. Basi akamwambia mwenzake naye akibishana naye: Mimi nimekushinda wewe kwa mali na nguvu za watu!
 
35Na akaingia kitaluni kwake, naye hali anajidhulumu nafsi yake. Akasema: Sidhani kabisa kuwa haya yataharibika.
 
36Wala sidhani kuwa hiyo Saa (ya Kyama) itatokea. Na ikiwa nitarudishwa kwa Mola wangu Mlezi, bila ya shaka nitapata marejeo bora zaidi kuliko haya.
 
37Mwenzake akamwambia kwa kubishana naye: Je! Unamkufuru aliye kuumba kutokana na udongo, tena kutokana na tone la manii, kisha akakufanya mtu kaamili?
 
38Lakini Yeye Mwenyezi Mungu ndiye Mola wangu Mlezi. Wala simshirikishi na yeyote.
 
39Na lau kuwa ulipo ingia kitaluni kwako ungeli sema: Mashaallah! Alitakalo Mwenyezi Mungu huwa! Hapana nguvu ila kwa Mwenyezi Mungu. Ikiwa unaniona mimi nina mali kidogo na watoto kuliko wewe,
 
40Basi huenda Mola wangu Mlezi akanipa kilicho bora kuliko kitalu chako, naye akapitisha kudra yake kutoka mbinguni kukilitea hicho chako, na kikageuka ardhi tupu inayo teleza.
 
41Au maji yake yakadidimia wala usiweze kuyagundua.
 
42Yakateketezwa matunda yake, akabaki akipindua pindua viganja vyake, kwa vile alivyo yagharimia, na miti imebwagika juu ya chanja zake. Akawa anasema: Laiti nisingeli mshiriki Mola wangu Mlezi na yeyote!
 
43Wala hakuwa nacho kikundi cha kumsaidia badala ya Mwenyezi Mungu, wala mwenyewe hakuweza kujisaidia.
 
44Huko ulinzi ni wa Mwenyezi Mungu wa Haki tu. Yeye ndiye mbora wa malipo, na mbora wa matokeo.
 
45Na wapigie mfano wa maisha ya dunia. Hayo ni kama maji tunayo yateremsha kutoka mbinguni, yakachanganyika na mimea ya ardhi, kisha hiyo mimea ikawa vibuwa vinavyo peperushwa na upepo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.
 
46Mali na wana ni pambo la maisha ya dunia. Na mema yanayo bakia ni bora mbele ya Mola wako Mlezi kwa malipo, na bora kwa matumaini.
 
47Na siku tutapo iondoa milima na ukaiona ardhi iwazi, na tukawafufua - wala hatutamwacha hata mmoja kati yao -
 
48Na wakahudhurishwa mbele ya Mola wako Mlezi kwa safu (wakaambiwa): Mmetujia kama tulivyo kuumbeni mara ya kwanza! Bali mlidai kwamba hatutakuwekeeni miadi.
 
49Na kitawekwa kitabu. Basi utawaona wakosefu wanavyo ogopa kwa yale yaliomo humo. Na watasema: Ole wetu! Kitabu hichi kina nini! Hakiachi dogo wala kubwa ila huliandika? Na watayakuta yote waliyo yatenda yamehudhuria hapo. Na Mola wako Mlezi hamdhulumu yeyote.
 
50Na tulipo waambia Malaika: Msujudieni Adam! Walimsjudia isipo kuwa Iblisi. Yeye alikuwa miongoni mwa majini, na akavunja amri ya Mola wake Mlezi. Je! Mnamshika yeye na dhuriya zake kuwa marafiki badala yangu, hali wao ni adui zenu? Ni ovu mno badala hii kwa wenye kudhulumu.
 
51Sikuwashuhudisha kuumbwa kwa mbingu na ardhi, wala kuumbwa kwa nafsi zao. Wala sikuwafanya wapotezao kuwa ni wasaidizi.
 
52Na siku atakapo sema (Mwenyezi Mungu): Waiteni hao mlio dai kuwa ni washirika wangu. Basi watawaita, na wao hawato waitikia. Nasi tutaweka baina yao maangamio.
 
53Na wakhalifu watauona Moto na watajua ya kwamba wao lazima wataingia humo; wala hawatapata pa kuuepuka.
 
54Na bila ya shaka tumewaelezea watu katika hii Qur'ani kila namna ya mfano. Lakini mwanaadamu amezidi kuliko kila kitu kwa ubishi.
 
55Na hapana kilicho wazuia watu kuamini ulipo wajia uwongofu na wakaomba maghfira kwa Mola wao Mlezi, isipo kuwa yawafikie ya wale wa zamani, au iwafikie adhabu jahara.
 
56Na hatuwatumi Mitume ila wawe wabashiri na waonyaji. Na walio kufuru wanabishana kwa uwongo, ili kwa uwongo huo waivunje kweli. Na wanazifanya Ishara zangu na yale waliyo onywa kuwa ni mzaha.
 
57Na ni nani dhaalimu mkubwa zaidi kuliko yule anaye kumbushwa Ishara za Mola wake Mlezi, naye akazipuuza na akasahau yaliyo tangulizwa na mikono yake? Hakika Sisi tumeweka vifuniko juu ya nyoyo zao ili wasifahamu, na uziwi kwenye masikio yao. Na ukiwaita kwenye uwongofu hawakubali kabisa kuongoka.
 
58Na Mola wako Mlezi ni Msamehevu Mwenye rehema. Lau angeli wachukulia kwa mujibu waliyo yachuma, bila ya shaka angeli wafanyia haraka kuwaadhibu. Lakini wanayo miadi ambayo hawatapata makimbilio yoyote ya kuepukana nayo.
 
59Na miji hiyo tuliwaangamiza watu wake walipo dhulumu. Na tukawawekea miadi ya maangamizo yao.
 
60Na pale Musa alipo mwambia kijana wake: Sitoacha kuendelea mpaka nifike zinapo kutana bahari mbili, au nitaendelea kwa muda mrefu.
 
61Basi wawili hao walipo fika zinapo kutana hizo bahari mbili walimsahau samaki wao, naye akashika njia yake kaporonyokea baharini.
 
62Walipo kwisha pita alimwambia kijana wake: Tupe chakula chetu cha mchana. Kwa hakika tumepata machofu kweli kwa hii safari yetu.
 
63Akasema (kijana): Waona! Pale tulipo pumzika penye jabali basi mimi nilimsahau yule samaki. Na hapana aliye nisahaulisha nisimkumbuke ila Shet'ani tu. Naye akashika njia yake baharini kwa ajabu.
 
64(Musa) akasema: Hayo ndiyo tuliyo kuwa tunayataka. Basi wakarudi nyuma kwa kufuata njia waliyo jia.
 
65Basi wakamkuta mja katika waja wangu tuliye mpa rehema kutoka kwetu, na tukamfunza mafunzo yaliyo toka kwetu.
 
66Musa akamwambia: Nikufuate ili unifunze katika ule uwongofu ulio funzwa wewe?
 
67Akasema: Hakika wewe hutaweza kuvumilia kuwa pamoja nami.
 
68Na utawezaje kuvumilia yale usiyo yajua vilivyo undani wake?
 
69Akasema: Inshaallah, Mwenyezi Mungu akipenda, utaniona mvumilivu, wala sitoasi amri yako.
 
70Akasema: Basi ukinifuata usiniulize kitu mpaka mimi nianze kukutajia.
 
71Basi wawili hao wakatoka, hata walipo panda jahazi (yule mtu) akaitoboa. (Musa) akasema: Unaitoboa uwazamishe watu wake? Hakika umefanya jambo baya.
 
72Akasema: Sikukwambia hutaweza kuvumilia kuwa pamoja nami?
 
73(Musa) akasema: Usinichukulie kwa niliyo sahau, wala usinipe uzito kwa jambo langu.
 
74Basi wakatoka wawili hao mpaka wakamkuta kijana, akamuuwa. (Musa) akasema: Ala! Umemuuwa mtu asiye na kosa, na wala hakuuwa! Ama hakika umefanya jambo baya kabisa!
 
75AKASEMA: Je! Sikukwambia kwamba hakika wewe huwezi kuvumilia kuwa pamoja nami?
 
76Akasema: Nikikuuliza kitu chochote baada ya haya usifuatane nami, kwani umekwisha pata udhuru kwangu.
 
77Basi wakatoka mpaka wakawafikia watu wa mji mmoja. Wakawaomba watu wake wawape chakula, nao wakakataa kuwakaribisha. Hapo wakakuta ukuta unataka kuanguka, (yule mja mwema) akausimamisha. (Musa) akasema: Ungeli taka ungeli chukua ujira kwa haya.
 
78(Yule mtu) akasema: Huku ndio kufarikiana baina yangu na wewe. Sasa nitakueleza maana ya yale uliyo kuwa huwezi kuyastahamilia.
 
79Ama ile jahazi ilikuwa ya masikini za Mungu wafanyao kazi baharini. Nilitaka kuiharibu, kwani nyuma yao alikuwako mfalme anaghusubu majahazi yote.
 
80Na ama yule kijana, wazazi wake walikuwa ni Waumini. Tukakhofu asije watia mashakani kwa uasi na ukafiri.
 
81Basi tulitaka Mola wao Mlezi awabadilishie aliye bora zaidi kuliko huyo kwa kutakasika, na aliye karibu zaidi kwa huruma.
 
82Na ama ukuta, huo ulikuwa ni wa vijana wawili mayatima kule mjini. Na chini yake ilikuwako khazina yao; na baba yao alikuwa ni mtu mwema. Basi Mola wako Mlezi alitaka wafikie utu uzima na wajitolee khazina yao wenyewe, kuwa ni rehema itokayo kwa Mola wako Mlezi. Wala mimi sikutenda hayo kwa amri yangu. Hiyo ndiyo tafsiri ya hayo ambayo wewe hukuweza kuyasubiria.
 
83Na wanakuuliza khabari za Dhul- Qarnaini. Waambie: Nitakusimulieni baadhi ya hadithi yake.
 
84Sisi tulimtilia nguvu katika ardhi na tukampa njia za kila kitu.
 
85Basi akaifuata njia.
 
86Hata alipo fika machwea-jua aliliona linatua katika checmchem yenye matope meusi. Na hapo akawakuta watu. Tukasema: Ewe Dhul-Qarnaini! Ama uwaadhibu au watwae kwa wema.
 
87Akasema: Ama aliye dhulumu basi tutamuadhibu, na kisha atarudishwa kwa Mola wake Mlezi amuadhibu adhabu isiyo juulikana.
 
88Na ama aliye amini na akatenda mema basi atapata malipo mazuri. Nasi tutamwambia lilio jepesi katika amri yetu.
 
89Kisha akaifuata njia.
 
90Hata alipo fika matokeo ya jua aliliona linawachomozea watu tusio wawekea pazia la kuwakinga nalo.
 
91Ndio hivyo hivyo. Na Sisi tulizijua vilivyo khabari zake zote.
 
92Kisha akaifuata njia.
 
93Hata alipo fika baina ya milima miwili, alikuta nyuma yake watu ambao takriban hawakuwa wanafahamu lolote.
 
94Wakasema: Ewe Dhul-Qarnaini! Hakika Juju-wa-maajuju wanafanya uharibifu katika nchi. Basi je, tukulipe ujira ili utujengee baina yetu na wao ngome?
 
95Akasema: Yale Mola wangu aliyo niwezesha ni bora zaidi. Lakini nyinyi nisaidieni kwa nguvu zenu. Nitakujengeeni kizuizi baina yenu na wao.
 
96Nileteeni vipande vya chuma. Hata alipo ijaza nafasi iliyo kati ya milima miwili, akasema: Vukuteni. Hata alipo kifanya (chuma) kama moto akasema: Nileteeni shaba iliyo yayuka niimwagie.
 
97Basi hawakuweza kuukwea, wala hawakuweza kuutoboa.
 
98Akasema: Hii ni rehema itokayo kwa Mola wangu Mlezi. Na itapo fika ahadi ya Mola wangu Mlezi atauvunja vunja. Na ahadi ya Mola wangu Mlezi ni kweli tu.
 
99Na siku hiyo tutawaacha wakisongana wao kwa wao. Na baragumu litapulizwa, na wote watakusanywa pamoja.
 
100Na siku hiyo tutawadhihirishia wazi Jahannamu makafiri waione.
 
101Wale ambao kwamba macho yao yalikuwa paziani hayanikumbuki, na wakawa hawawezi kusikia.
 
102Je, wanadhani walio kufuru ndio wawafanye waja wangu ndio walinzi wao badala yangu Mimi? Hakika Sisi tumeiandaa Jahannamu iwe ndipo mahala pa kuteremkia makafiri.
 
103Sema: Je, tukutajieni wenye khasara mno katika vitendo vyao?
 
104Ni wale ambao juhudi yao katika maisha ya dunia imepotea bure, nao wanadhani kwamba wanafanya kazi nzuri.
 
105Hao ni wale walio zikanusha Ishara za Mola wao Mlezi na kukutana naye. Kwa hivyo vitendo vyao vimepotea bure, na wala Siku ya Kiyama hatutawathamini kitu.
 
106Hiyo Jahannamu ni malipo yao kwa walivyo kufuru na wakafanyia kejeli Ishara zangu na Mitume wangu.
 
107Hakika wale walio amini na wakatenda mema mashukio yao yatakuwa kwenye Pepo za Firdausi.
 
108Watadumu humo; hawatataka kuondoka.
 
109Sema: Lau kuwa bahari ndio wino kwa maneno ya Mola wangu Mlezi, basi bahari ingeli malizika kabla ya kumalizika maneno ya Mola wangu Mlezi, hata tungeli ileta mfano wa hiyo kuongezea.
 
110Sema: Mimi ni mwanaadamu kama nyinyi. Ninaletewa Wahyi kwamba Mungu wenu ni Mungu Mmoja. Mwenye kutaraji kukutana na Mola wake Mlezi basi naatende vitendo vyema, wala asimshirikishe yeyote katika ibada ya Mola wake Mlezi.
 
 
ReadTheQuran.org