Translations Suras
KISWAHILI

43 - AZZUKHRUF

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.

 
1H'a Mim
 
2Naapa kwa Kitabu kinacho bainisha.
 
3Hakika Sisi tumeifanya Qur'ani kwa Kiarabu ili mfahamu.
 
4Na hakika hiyo imo katika Asili ya Maandiko yalioko kwetu, ni tukufu na yenye hikima.
 
5Je! Tuache kukukumbusheni kabisa kwa kuwa nyinyi ni watu mlio pita mipaka kwa ukafiri?
 
6Na Manabii wangapi tuliwatuma kwa watu wa zamani!
 
7Na hawajii Nabii yeyote ila walikuwa wakimkejeli.
 
8Na tuliwaangamiza walio kuwa na nguvu kushinda wao. Na mfano wa watu wa zamani umekwisha pita.
 
9Na ukiwauliza: Nani aliye ziumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka watasema: Kaziumba Mwenye nguvu, Mjuzi,
 
10Ambaye amekufanyieni ardhi kama tandiko, na akakufanyieni ndani yake njia mpate kuongoka.
 
11Na ambaye ndiye aliye teremsha kutoka mbinguni maji kwa kiasi, na kwa hayo tukaifufua nchi iliyo kufa. Na namna hivi ndivyo mtakavyo tolewa.
 
12Na ambaye ndiye aliye umba katika kila kitu jike na dume, na akakufanyieni marikebu na wanyama mnao wapanda.
 
13Ili mkae vizuri migongoni mwao, kisha mkumbuke neema za Mola wenu Mlezi mnapokaa sawa sawa juu yao na mseme: Ametakasika aliye mfanya huyu atutumikie, na tusingeli weza kufanya haya wenyewe.
 
14Na hakika sisi tutarudi kwa Mola wetu Mlezi.
 
15Na wanamfanyia katika waja wake fungu. Kwa hakika mwanaadamu ni mtovu wa fadhila aliye dhaahiri.
 
16Au amejichukulia watoto wanawake katika vile alivyo viumba, na akakuteulieni nyinyi watoto wanaume?
 
17Na anapo bashiriwa mmoja wao kwa yale aliyo mpigia mfano Mwenyezi Mungu, uso wake husawijika na hujaa hasira.
 
18Ati aliye lelewa katika mapambo, na katika mabishano hawezi kusema kwa bayana...?
 
19Na wakawafanya Malaika, ambao ni waja wa Mwingi wa Rehema, ni wanawake! Kwani wameshuhudia kuumbwa kwao? Ushahidi wao utaandikwa na wao watahojiwa!
 
20Nao husema: Angeli penda Mwingi wa Rehema tusingeli waabudu sisi. Hawana ujuzi wowote wa hayo! Hawana ila kusema uwongo tu!
 
21Kwani tuliwapa Kitabu kabla ya hichi, na ikawa wao wanakishikilia hicho?
 
22Bali wanasema: Hakika sisi tuliwakuta baba zetu wanashika dini makhsusi, basi na sisi tunaongoza nyayo zao.
 
23Na kadhaalika hatukumtuma mwonyaji kwenye mji wowote ila watu wake walio deka kwa starehe walisema: Hakika sisi tuliwakuta baba zetu wanashika dini makhsusi, na sisi tunafuata nyayo zao.
 
24Akasema (Mwonyaji): Hata nikikuleteeni yenye uwongofu bora kuliko mlio wakuta nao baba zenu? Wakasema: Sisi tunayakataa tu hayo mliyo tumwa.
 
25Basi tukawalipizia. Angalia ulikuwaje mwisho wa walio kadhibisha!
 
26Na pale Ibrahim alipo mwambia baba yake na kaumu yake: Hakika mimi ninajitenga mbali na hayo mnayo yaabudu,
 
27Isipo kuwa yule aliye niumba, kwani Yeye ataniongoa.
 
28Na akalifanya hili liwe neno lenye kubaki katika vizazi vyake ili warejee.
 
29Bali tuliwastarehesha hawa na baba zao mpaka ikawafikia Haki na Mtume aliye bainisha.
 
30Na ilipo wafikia Haki wakasema: Huu ni uchawi, na sisi hakika tunaukataa.
 
31Na walisema: Kwa nini Qur'ani hii haikuteremshwa kwa mtu mkubwa katika miji miwili hii?
 
32Kwani wao ndio wanao gawa rehema za Mola wako Mlezi? Sisi tumewagawanyia baina yao maisha yao katika uhai wa duniani, na tukawanyanyua baadhi yao juu ya wengine kwa daraja nyingi; kwa hivyo baadhi yao wanawafanya wenginewe wawatumikie. Na rehema za Mwenyezi Mungu ni bora kuliko hayo wanayo yakusanya.
 
33Na lau isinge kuwa watu watakuwa kundi moja tungeli wajaalia wanao mkufuru Rahmani wana nyumba zao zina dari ya fedha, na ngazi zao pia wanazo pandia,
 
34Na milango ya nyumba zao na vitanda wanavyo egemea juu yake,
 
35Na mapambo. Lakini hayo si chochote ila ni starehe ya maisha ya dunia tu, na Akhera iliyoko kwa Mola wako Mlezi ni ya wenye kumchamngu.
 
36Anaye yafanyia upofu maneno ya Rahmani tunamwekea Shet'ani kuwa ndiye rafiki yake.
 
37Na hakika wao wanawazuilia Njia na wenyewe wanadhani kuwa wameongoka.
 
38Hata atakapo tujia atasema: Laiti ungeli kuwako baina yangu na wewe kama umbali baina ya mashariki na magharibi. Rafiki mwovu mno wewe!
 
39Na kwa kuwa mlidhulumu, haitakufaeni kitu leo kwamba nyinyi mnashirikiana katika adhabu.
 
40Je! Unaweza kuwasikilizisha viziwi, au unaweza kuwaongoa vipofu na waliomo katika upotofu ulio wazi?
 
41Na hata tukikuondoa, Sisi tutalipiza kisasi chetu kwao.
 
42Au tutakuonyesha tulio waahidi. Nasi bila ya shaka tuna uweza juu yao.
 
43Basi wewe yashike yaliyo funuliwa kwako. Hakika wewe uko kwenye Njia Iliyo Nyooka.
 
44Na hakika haya ni ukumbusho kwako na kwa kaumu yako. Na mtakuja ulizwa.
 
45Na waulize Mitume wetu tulio watuma kabla yako: Je! Tulifanya miungu mingine iabudiwe badala ya Rah'mani?
 
4646, Na bila ya shaka tulimtuma Musa kwa Ishara zetu ende kwa Firauni na waheshimiwa wake, na akasema: Hakika mimi ni Mtume wa Mola Mlezi wa walimwengu wote!
 
47Lakini alipo wajia na Ishara zetu wakaingia kuzicheka.
 
48Na hatukuwaonyesha Ishara yoyote ila hiyo ilikuwa kubwa zaidi kuliko nyenginewe. Na tukawakamata kwa adhabu ili warejee.
 
49Na wakasema: Ewe mchawi! Tuombee kwa Mola wako Mlezi kwa ile ahadi aliyo kuahidi; hakika sisi tutakuwa wenye kuongoka.
 
50Basi tulipo waondolea adhabu hiyo, mara wakaingia kuvunja ahadi.
 
51Na Firauni alitangaza kwa watu wake, akisema: Enyi watu wangu! Kwani mimi sinao huu ufalme wa Misri, na hii mito inapita chini yangu? Je! Hamwoni?
 
52Au mimi si bora kuliko huyu aliye mnyonge, wala hawezi kusema waziwazi?
 
53Basi mbona hakuvikwa vikuku vya dhahabu, au hawakuja Malaika pamoja naye wakamwandama?
 
54Basi aliwachezea watu wake, na wakamt'ii. Kwa hakika hao walikuwa watu wapotovu.
 
55Walipo tukasirisha tuliwapatiliza tukawazamisha wote!
 
56Kisha tukawafanya kuwa watangulizi na mfano kwa wa baadaye.
 
57Na alipo pigiwa mfano Mwana wa Mariamu, watu wako waliupiga ukelele.
 
58Wakasema: Miungu yetu kwani si bora kuliko huyu? Hawakukupigia mfano huo ila kwa ubishi tu. Bali hao ni watu wagomvi!
 
59Hakuwa yeye (Isa) ila ni Mtumwa tuliye mneemesha na tukamfanya ni mfano kwa Wana wa Israili.
 
60Na tungeli penda tungeli wafanyia miongoni mwenu Malaika katika ardhi wakifuatana.
 
61Na kwa hakika yeye ni alama ya Saa ya Kiyama. Basi usiitilie shaka, na nifuateni. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka.
 
62Wala asikuzuilieni Shet'ani. Hakika yeye ni adui yenu wa dhaahiri.
 
63Na alipo kuja Isa na dalili zilizo wazi, alisema: Nimekujieni na hikima, na ili nikuelezeni baadhi ya yale mliyo khitalifiana. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na mnit'ii mimi.
 
64Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu Mlezi, na ni Mola wenu Mlezi. Basi Muabuduni Yeye tu. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka.
 
65Lakini makundi kwa makundi yao yalikhitalifiana wao kwa wao. Ole wao walio dhulumu kwa adhabu ya siku chungu.
 
66Je! Nini wanangojea ila Saa iwajie kwa ghafla na wala wao hawatambui?
 
67Siku hiyo marafiki watakuwa ni maadui, wao kwa wao, isipo kuwa wachamngu.
 
68Enyi waja wangu! Hamtakuwa na khofu siku hiyo, wala hamtahuzunika.
 
69Ambao waliziamini Ishara zangu na walikuwa Waislamu.
 
70Ingieni Peponi, nyinyi na wake zenu; mtafurahishwa humo.
 
71Watakuwa wanapitishiwa sahani za dhahabu na vikombe; na vitakuwamo ambavyo nafsi zinavipenda na macho yanavifurahia, na nyinyi mtakaa humo milele.
 
72Na hiyo ni Pepo mliyo rithishwa kwa hayo mliyo kuwa mkiyafanya.
 
73Mnayo humo matunda mengi mtakayo yala.
 
74Kwa hakika wakosefu watakaa katika adhabu ya Jahannamu.
 
75Hawatapumzishwa nayo na humo watakata tamaa.
 
76Wala Sisi hatukuwadhulumu, bali wao ndio walio kuwa madhaalimu.
 
77Nao watapiga kelele waseme: Ewe Malik! Na atufishe Mola wako Mlezi! Naye aseme: Hakika nyinyi mtakaa humo humo!
 
78Kwa yakini tulikuleteeni Haki, lakini wengi katika nyinyi mlikuwa mnaichukia Haki.
 
79Au waliweza kupitisha amri yao? Bali ni Sisi ndio tunao pitisha.
 
80Au wanadhani kwamba hatusikii siri zao na minong'ono yao? Wapi! Na wajumbe wetu wapo karibu nao, wanayaandika.
 
81Sema: Ingeli kuwa Rahmani ana mwana, basi mimi ningeli kuwa wa kwanza kumuabudu.
 
82Ametakasika Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, Mola Mlezi wa A'rshi, na hayo wanayo msifia.
 
83Basi waache wapige porojo wakicheza mpaka wakutwe na hiyo siku yao waliyo ahidiwa.
 
84Na Yeye ndiye Mungu mbinguni, na ndiye Mungu katika ardhi. Naye ndiye Mwenye hikima, Mwenye ujuzi.
 
85Na ametukuka Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi na viliomo ndani yake. Na uko kwake ujuzi wa Saa ya Kiyama, na kwake Yeye mtarudishwa.
 
86Wala hao mnao waomba badala yake Yeye hawana uweza wa kumwombea mtu, isipo kuwa anaye shuhudia kwa haki, na wao wanajua.
 
87Na ukiwauliza ni nani aliye waumba? Bila ya shaka watasema: Mwenyezi Mungu! Basi ni wapi wanako geuziwa?
 
88Na usemi wake (Mtume) ni: Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika hawa ni watu wasio amini.
 
89Basi wasamehe, na uwambie maneno ya salama. Watakuja jua.
 
 
ReadTheQuran.org