Translations | Suras |
KISWAHILI | |
50 - QAAF | |
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU. | |
1 | Qaaf. Naapa kwa Qur'ani tukufu! |
2 | Bali wanastaajabu kwamba amewafikia mwonyaji kutoka miongoni mwao, na wakasema makafiri: Hili ni jambo la ajabu! |
3 | Ati tukifa na tukawa udongo...? Kurejea huko kuko mbali! |
4 | Hakika Sisi tunajua kiasi cha kila kinacho punguzwa na ardhi kutokana nao. Na kwetu kipo Kitabu kinacho hifadhi yote. |
5 | Lakini waliikanusha Haki ilipo wajia; kwa hivyo wamo katika mambo ya mkorogo. |
6 | Je! Hawaangalii mbingu zilizo juu yao! Vipi tulivyo zijenga, na tukazipamba. Wala hazina nyufa. |
7 | Na ardhi tumeitandaza na tukaiwekea milima, na tukaiotesha mimea mizuri ya kila namna. |
8 | Yawe haya ni kifumbua macho na ukumbusho kwa kila mja mwenye kuelekea. |
9 | Na tumeteremsha kutoka mbinguni maji yaliyo barikiwa, na kwa hayo tukaotesha mabustani na nafaka za kuvunwa. |
10 | Na mitende mirefu yenye makole yaliyo zaa kwa wingi, |
11 | Ili iwe ni riziki kwa waja wangu. Na tukaifufua kwa maji nchi iliyo kuwa imekufa. Kama hivyo ndivyo utakavyo kuwa ufufuaji. |
12 | Kabla yao walikadhibisha kaumu ya Nuhu na wakaazi wa Rassi na Thamudi. |
13 | Na A'di na Firauni na kaumu ya Lut'i. |
14 | Na wakaazi wa Machakani, na watu wa Tubbaa'. Wote hao waliwakanusha Mitume, kwa hivyo onyo likathibitika juu yao. |
15 | Kwani tulichoka kwa kuumba mara ya kwanza. Bali wao wamo katika shaka tu juu ya umbo jipya. |
16 | Na hakika tumemuumba mtu, nasi tunayajua yanayo mpitikia katika nafsi yake. Na Sisi tuko karibu naye kuliko mshipa wa shingoni mwake. |
17 | Wanapo pokea wapokeaji wawili, wanao kaa kuliani na kushotoni. |
18 | Hatamki neno ila karibu yake yupo mwangalizi tayari. |
19 | Na uchungu wa kutoka roho utamjia kwa haki. Hayo ndiyo uliyo kuwa ukiyakimbia. |
20 | Na litapulizwa baragumu. Hiyo ndiyo Siku ya Miadi. |
21 | Na kila nafsi itakuja na pamoja nayo mchungaji na shahidi. |
22 | (Aambiwe): Kwa hakika ulikuwa umeghafilika na haya; basi leo tumekuondolea pazia lako, na kwa hivyo kuona kwako leo ni kukali. |
23 | Na mwenzake atasema: Huyu niliye naye mimi kesha tayarishwa. |
24 | Mtupeni katika Jahannamu kila kafiri mwenye inda, |
25 | Akatazaye kheri, arukaye mipaka, mwenye kutia shaka, |
26 | Aliye weka mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu. Basi mtupeni katika adhabu kali. |
27 | Mwenzake aseme: Ee Mola wetu Mlezi! Sikumpoteza mimi, bali yeye mwenyewe alikuwa katika upotovu wa mbali. |
28 | (Mwenyezi Mungu) aseme: Msigombane mbele yangu. Nilikuleteeni mbele onyo langu. |
29 | Mbele yangu haibadilishwi kauli, wala Mimi siwadhulumu waja wangu. |
30 | Siku tutapo iambia Jahannamu: Je! Umejaa? Nayo itasema: Je! Kuna ziada? |
31 | Na Pepo italetwa karibu kwa ajili ya wachamngu, haitakuwa mbali. |
32 | Haya ndiyo mnayo ahidiwa kwa kila mwenye kurejea kwa Mwenyezi Mungu na akajilinda. |
33 | Mwenye kumwogopa Mwingi wa Rehema hali kuwa hamwoni, na akaja kwa moyo ulio elekea- |
34 | (Ataambiwa) ingieni kwa salama. Hiyo ndiyo siku ya daima dawamu. |
35 | Humo watapata wakitakacho, na kwetu yako ya ziada. |
36 | Na kaumu ngapi tuliziangamiza kabla yao walio kuwa na nguvu zaidi kuliko hawa! Nao walitanga tanga katika nchi nyingi. Je! Walipata pa kukimbilia? |
37 | Hakika katika hayo upo ukumbusho kwa mwenye moyo au akatega sikio naye yupo anashuhudia. |
38 | Na bila ya shaka Sisi tumeziumba mbingu na ardhi na vilio baina yao mnamo siku sita; na wala hayakutugusa machofu. |
39 | Basi vumilia kwa hayo wasemayo, na mtakase kwa kumsifu Mola wako Mlezi kabla ya kuchomoza jua na kabla ya kuchwa. |
40 | Na katika usiku pia mtakase, na baada ya kusujudu. |
41 | Na sikiliza siku atapo nadi mwenye kunadi kutoka pahala karibu. |
42 | Siku watakapo sikia ukelele wa haki. Hiyo ndiyo siku ya kufufuka. |
43 | Hakika Sisi tunahuisha na tunafisha, na kwetu Sisi ndio marejeo. |
44 | Siku itapo wapasukia ardhi mbio mbio! Mkusanyo huo kwetu ni mwepesi. |
45 | Sisi tunajua kabisa wayasemayo. Wala wewe si mwenye kuwatawalia kwa ujabari. Basi mkumbushe kwa Qur'ani anaye liogopa onyo. |
ReadTheQuran.org |