Translations Suras
KISWAHILI

56 - AL -WAAQIA'H

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.

 
1Litakapo tukia hilo Tukio
 
2Hapana cha kukanusha kutukia kwake.
 
3Literemshalo linyanyualo,
 
4Itakapo tikiswa ardhi kwa mtikiso,
 
5Na milima itapo sagwasagwa,
 
6Iwe mavumbi yanayo peperushwa,
 
7Na nyinyi mtakuwa namna tatu:-
 
8Basi watakuwepo wa kuliani; je, ni wepi wa kuliani?
 
9Na wa kushotoni; je, ni wepi wa kushotoni?
 
10Na wa mbele watakuwa mbele.
 
11Hao ndio watakao karibishwa
 
12Katika Bustani zenye neema.
 
13Fungu kubwa katika wa mwanzo,
 
14Na wachache katika wa mwisho.
 
15Watakuwa juu ya viti vya fakhari vilivyo tonewa.
 
16Wakiviegemea wakielekeana.
 
17Wakitumikiwa na wavulana wa ujana wa milele,
 
18Kwa vikombe na mabirika na bilauri za vinywaji kutoka chemchem safi.
 
19Hawataumwa kichwa kwa vinywaji hivyo wala hawatoleweshwa.
 
20Na matunda wayapendayo,
 
21Na nyama za ndege kama wanavyo tamani.
 
22Na Mahurulaini,
 
23Walio kama mfano wa lulu zilio hifadhiwa.
 
24Ni malipo kwa waliyo kuwa wakiyatenda.
 
25Humo hawatasikia porojo wala maneno ya dhambi,
 
26Isipo kuwa maneno ya Salama, Salama.
 
27Na wale wa mkono wa kulia, ni yepi yatakuwa ya wa kuliani?
 
28Katika mikunazi isiyo na miba,
 
29Na migomba iliyo pangiliwa,
 
30Na kivuli kilicho tanda,
 
31Na maji yanayo miminika,
 
32Na matunda mengi,
 
33Hayatindikii wala hayakatazwi,
 
34Na matandiko yaliyo nyanyuliwa.
 
35Hakika Sisi tutawaumba (Mahurulaini) upya,
 
36Na tutawafanya vijana,
 
37Wanapendana na waume zao, hirimu moja.
 
38Kwa ajili ya watu wa kuliani.
 
39Fungu kubwa katika wa mwanzo,
 
40Na fungu kubwa katika wa mwisho. 3
 
41Na watu wa kushotoni; je ni yepi ya wa kushotoni?
 
42Katika upepo wa moto, na maji yanayo chemka,
 
43Na kivuli cha moshi mweusi,
 
44Si cha kuburudisha wala kustarehesha.
 
45Hakika hao walikuwa kabla ya haya wakiishi maisha ya anasa.
 
46Na walikuwa wakishikilia kufanya madhambi makubwa,
 
47Na walikuwa wakisema: Tutakapo kufa na tukawa udongo na mafupa, ati ndio tutafufuliwa?
 
48Au baba zetu wa zamani?
 
49Sema: Hakika wa zamani na wa mwisho
 
50Bila ya shaka watakusanywa kwa wakati wa siku maalumu.
 
51Kisha nyinyi, mlio potea, mnao kanusha,
 
52Kwa yakini mtakula mti wa Zaqqumu.
 
53Na kwa mti huo mtajaza matumbo.
 
54Na juu yake mtakunywa maji yanayo chemka.
 
55Tena mtakunywa kama wanavyo kunywa ngamia wenye kiu.
 
56Hiyo ndiyo karamu yao Siku ya Malipo.
 
57Sisi tumekuumbeni; basi hamsadiki?
 
58Je! Mnaiona mbegu ya uzazi mnayo idondokeza?
 
59Je! Mnaiumba nyinyi, au ni Sisi ndio Waumbaji?
 
60Sisi tumekuwekeeni mauti; na wala Sisi hatushindwi
 
61Kuwaleta wengine badala yenu na kukuumbeni nyinyi kwa umbo msilo lijua.
 
62Na bila ya shaka mlikwisha jua umbo la kwanza, basi kwa nini hamkumbuki?
 
63Je! Mnaona makulima mnayo yapanda?
 
64Je! Ni nyinyi mnayo yaotesha au ni Sisi ndio wenye kuotesha?
 
65Tungeli taka tungeli yafanya yakawa mapepe, mkabaki mnastaajabu,
 
66Mkisema: Hakika sisi tumegharimika;
 
67Bali sisi tumenyimwa.
 
68Je! Mnayaona maji mnayo yanywa?
 
69Je! Ni nyinyi mnayo yateremsha kutoka mawinguni au ni Sisi ndio wenye kuyateremsha?
 
70Tungeli penda tungeli yafanya ya chumvi. Basi mbona hamshukuru?
 
71Je! Mnauona moto mnao uwasha?
 
72Ni nyinyi mlio uumba mti wake au Sisi ndio Waumbaji?
 
73Sisi tumeufanya uwe ni ukumbusho na manufaa kwa walioko nyikani.
 
74Basi litakase jina la Mola wako Mlezi aliye Mkuu.
 
75Basi naapa kwa maanguko ya nyota,
 
76Na hakika bila ya shaka hichi ni kiapo kikubwa, laiti mngeli jua!
 
77Hakika hii bila ya shaka ni Qur'ani Tukufu,
 
78Katika Kitabu kilicho hifadhiwa.
 
79Hapana akigusaye ila walio takaswa.
 
80Ni uteremsho unao toka kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
 
81Ni maneno haya ndiyo nyinyi mnayapuuza?
 
82Na badala ya kushukuru kwa riziki yenu mnafanya kuwa mnakadhibisha?
 
83Yawaje basi itakapo fika roho kwenye koo,
 
84Na nyinyi wakati huo mnatazama!
 
85Na Sisi tuko karibu zaidi naye kuliko nyinyi.
 
86Na lau kuwa nyinyi hamumo katika mamlaka yangu,
 
87Kwanini hamuirudishi hiyo roho, ikiwa nyinyi mnasema kweli?
 
88Basi akiwa miongoni mwa walio karibishwa,
 
89Basi ni raha, na manukato, na Bustani zenye neema.
 
90Na akiwa katika watu wa upande wa kulia,
 
91Basi ni Salamu kwako uliye miongoni mwa watu wa upande wa kulia.
 
92Na ama akiwa katika walio kadhibisha wapotovu,
 
93Basi karamu yake ni maji yanayo chemka,
 
94Na kutiwa Motoni.
 
95Hakika hii ndiyo haki yenye yakini.
 
96Basi litakase jina la Mola wako Mlezi aliye Mkubwa.
 
 
ReadTheQuran.org