36 - YA-SIN |
| |
|
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU. |
| |
| |
| 1 | Ya-Sin (Y.S.). |
| |
| 2 | Kwa Haki ya Qur'ani yenye hikima! |
| |
| 3 | Hakika wewe ni miongoni mwa walio tumwa, |
| |
| 4 | Juu ya Njia Iliyo Nyooka. |
| |
| 5 | Uteremsho wa Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu. |
| |
| 6 | Ili uwaonye watu ambao baba zao hawakuonywa , basi wao wamekuwa wenye kughafilika. |
| |
| 7 | Bila ya shaka kauli imekwisha thibiti juu ya wengi katika wao, kwa hivyo hawaamini. |
| |
| 8 | Tumeweka makongwa shingoni mwao, yakawafika videvuni. Kwa hivyo vichwa vyao viko juu tu. |
| |
| 9 | Tumeweka kizuizi mbele yao, na kizuizi nyuma yao, na tumewafunika macho yao; kwa hivyo hawaoni. |
| |
| 10 | Ni sawa sawa kwao ukiwaonya au usiwaonye, hawataamini. |
| |
| 11 | Hakika wewe unamwonya mwenye kufuata ukumbusho, na akamcha Arrahman, Mwingi wa Rehema, kwa ghaibu. Basi mbashirie huyo msamaha na ujira mwema. |
| |
| 12 | Hakika Sisi tunawafufua wafu, na tunayaandika wanayo yatanguliza, na wanayo yaacha nyuma. Na kila kitu tumekihifadhi katika daftari asli lenye kubainisha. |
| |
| 13 | Na wapigie mfano wa wakaazi wa mji walipo wafikia walio tumwa. |
| |
| 14 | Tulipo watumia wawili, wakawakanusha. Basi tukawazidishia nguvu kwa mwingine wa tatu. Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwenu. |
| |
| 15 | Wakasema: Nyinyi si chochote ila ni watu kama sisi. Na Mwingi wa Rehema hakuteremsha kitu. Nyinyi mnasema uwongo tu. |
| |
| 16 | Wakasema: Mola wetu Mlezi anajua kwamba hakika sisi tumetumwa kwenu. |
| |
| 17 | Wala si juu yetu ila kufikisha ujumbe ulio wazi. |
| |
| 18 | Wakasema: Sisi tumeagua kuwa nyinyi ni wakorofi. Ikiwa hamtaacha basi kwa yakini tutakupigeni mawe, na mtapata adhabu chungu kutoka kwetu. |
| |
| 19 | Wakasema: Ukorofi wenu mnao wenyewe! Je! Ni kwa kuwa mnakumbushwa? Ama nyinyi ni watu walio pindukia mipaka. |
| |
| 20 | Na akaja mtu mbio kutokea upande wa mbali wa mjini, akasema: Enyi watu wangu! Wafuateni hawa walio tumwa. |
| |
| 21 | Wafuateni ambao hawakutakini ujira, hali ya kuwa wenyewe wameongoka. |
| |
| 22 | NA KWA NINI nisimuabudu yule aliye niumba na kwake mtarejeshwa? |
| |
| 23 | Je! Niishike miungu mingine badala yake? Arrahmani, Mwingi wa Rehema, akinitakia madhara uombezi wa hao hautanifaa kitu, wala hawataniokoa. |
| |
| 24 | Basi hakika mimi hapo nitakuwa katika upotovu ulio dhaahiri. |
| |
| 25 | Hakika mimi nimemuamini Mola wenu Mlezi, basi nisikilizeni! |
| |
| 26 | Akaambiwa: Ingia Peponi! Akasema: Laiti kuwa watu wangu wangeli jua |
| |
| 27 | Jinsi Mola wangu Mlezi alivyo nisamehe, na akanifanya miongoni mwa walio hishimiwa. |
| |
| 28 | Na hatukuwateremshia kaumu yake baada yake jeshi kutoka mbinguni, wala si wenye kuteremsha. |
| |
| 29 | Hakukuwa ila ukelele mmoja tu; na mara walizimwa! |
| |
| 30 | Nawasikitikia waja wangu. Hawajii Mtume ila wao humkejeli. |
| |
| 31 | Je! Hawaoni umma ngapi tulizo ziangamiza kabla yao? Hakika hao hawarejei tena kwao. |
| |
| 32 | Na hapana mmoja ila wote watakusanywa waletwe mbele yetu. |
| |
| 33 | Na Ishara hiyo kwao - ardhi iliyo kufa, nasi tukaifufua, na tukatoa ndani yake nafaka, wakawa wanazila! |
| |
| 34 | Na tukafanya ndani yake mabustani ya mitende na mizabibu, na tukatimbua chemchem ndani yake, |
| |
| 35 | Ili wale matunda yake, na hayo hayakufanywa na mikono yao! Basi je, hawashukuru? |
| |
| 36 | Subhana, Ametakasika, aliye umba dume na jike vyote katika vinavyo mea katika ardhi na katika nafsi zao, na katika wasivyo vijua. |
| |
| 37 | Na usiku ni Ishara kwao. Tunauvua humo mchana, mara wao wanakuwa gizani. |
| |
| 38 | Na jua linakwenda kwa kiwango chake. Hayo ni makadirio ya Mwenye nguvu, Mwenye kujua. |
| |
| 39 | Na mwezi tumeupimia vituo, mpaka unakuwa kama karara kongwe. |
| |
| 40 | Haliwi jua kuufikia mwezi, wala usiku kuupita mchana. Na vyote vinaogelea katika njia zao. |
| |
| 41 | Na ni Ishara kwao kwamba Sisi tuliwapakia dhuriya zao katika jahazi ilio sheheni. |
| |
| 42 | Na tukawaumbia kutoka mfano wake wanavyo vipanda. |
| |
| 43 | Na tukitaka tunawazamisha, wala hapana wa kuwasaidia, wala hawaokolewi, |
| |
| 44 | Isipo kuwa kwa rehema zitokazo kwetu na starehe kwa muda. |
| |
| 45 | Na wanapo ambiwa: Jilindeni na yalioko mbele yenu na yalioko nyuma yenu, ili mpate kurehemewa... |
| |
| 46 | Na haiwafikii Ishara yoyote katika Ishara za Mola wao Mlezi ila wao huwa ni wenye kuipuuza. |
| |
| 47 | Na wanapo ambiwa: Toeni katika aliyo kupeni Mwenyezi Mungu, walio kufuru huwaambia walio amini: Je! Tuwalishe ambao Mwenyezi Mungu angependa angeli walisha mwenyewe? Nyinyi hammo ila katika upotofu ulio dhaahiri. |
| |
| 48 | Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini, ikiwa nyinyi ni wakweli? |
| |
| 49 | Hawangojei ila ukelele mmoja tu utakao wachukua nao wamo kuzozana. |
| |
| 50 | Basi hawataweza kuusia, wala kwa watu wao hawarejei. |
| |
| 51 | Na litapulizwa barugumu, mara watatoka makaburini wakikimbilia kwa Mola wao Mlezi. |
| |
| 52 | Watasema: Ole wetu! Nani aliye tufufua kwenye malazi yetu? Haya ndiyo aliyo yaahidi Mwingi wa Rehema na wakasema kweli Mitume. |
| |
| 53 | Haitakuwa ila ukelele mmoja tu, mara wote watahudhuruishwa mbele yetu. |
| |
| 54 | Basi leo nafsi yoyote haitadhulumiwa kitu, wala hamtalipwa ila yale mliyo kuwa mkiyatenda. |
| |
| 55 | Hakika watu wa Peponi leo wamo shughulini, wamefurahi. |
| |
| 56 | Wao na wake zao wamo katika vivuli wameegemea juu ya viti vya fakhari. |
| |
| 57 | Watapata humo kila namna ya matunda na watapata kila watakacho kitaka. |
| |
| 58 | "Salama!" Hiyo ndiyo kauli itokayo kwa Mola Mlezi Mwenye kurehemu. |
| |
| 59 | Na enyi wakosefu! Jitengeni leo! |
| |
| 60 | Je! Sikuagana nanyi, enyi wanaadamu, kuwa msimuabudu Shet'ani? Hakika yeye ni adui dhaahiri kwenu. |
| |
| 61 | Na ya kwamba mniabudu Mimi? Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka. |
| |
| 62 | Na bila ya shaka yeye amekwisha lipoteza kundi kubwa miongoni mwenu. Je, hamkuwa mkifikiri? |
| |
| 63 | Hii basi ndiyo Jahannamu mliyo kuwa mkiahidiwa. |
| |
| 64 | Ingieni leo kwa vile mlivyo kuwa mkikufuru. |
| |
| 65 | Leo tunaviziba vinywa vyao, na iseme nasi mikono yao, na itoe ushahidi miguu yao kwa waliyo kuwa wakiyachuma. |
| |
| 66 | Na tungeli penda tungeli yafutilia mbali macho yao, wakawa wanaiwania njia. Lakini wange ionaje? |
| |
| 67 | Na tungeli taka tunge wageuza sura hapo hapo walipo, basi wasinge weza kwenda wala kurudi. |
| |
| 68 | Na tunaye mzeesha tunamrudisha nyuma katika umbo. Basi je! hawazingatii? |
| |
| 69 | Wala hatukumfundisha (Muhammad) mashairi, wala hayatakikani kwake hayo. Haukuwa huu ila ni ukumbusho na Qur'ani inayo bainisha. |
| |
| 70 | Ili imwonye aliye hai, na neno litimie juu ya makafiri. |
| |
| 71 | Je! Hawaoni kwamba tumewaumbia kutokana na iliyo fanya mikono yetu wanyama wa mifugo, na wao wakawa wenye kuwamiliki. |
| |
| 72 | Na Sisi tukawadhalilishia. Basi baadhi yao wako wanao wapanda, na baadhi yao wanawala. |
| |
| 73 | Na wao wanapata kwao manufaa na vinywaji. Basi je, hawashukuru? |
| |
| 74 | Na wameishika miungu mingine badala ya Mwenyezi Mungu ili ati wapate kusaidiwa! |
| |
| 75 | Hawataweza kuwasaidia. Bali hao ndio watakuwa askari wao watakao hudhurishwa. |
| |
| 76 | Basi maneno yao yasikuhuzunishe. Hakika Sisi tunayajua wanayo yaweka siri na wanayo yatangaza. |
| |
| 77 | Kwani mwanaadamu haoni ya kwamba Sisi tumemuumba yeye kutokana na tone la manii? Kisha sasa yeye ndio amekuwa ndiye mgomvi wa dhaahiri! |
| |
| 78 | Na akatupigia mfano, na akasahau kuumbwa kwake, akasema: Ni nani huyo atakaye ihuisha mifupa nayo imekwisha mung'unyika? |
| |
| 79 | Sema: Ataihuisha huyo huyo aliye iumba hapo mara ya mwanzo. Na Yeye ni Mjuzi wa kila kuumba. |
| |
| 80 | Aliye kujaalieni kupata moto kutokana na mti wa kijani nanyi mkawa kwa huo mnawasha. |
| |
| 81 | Kwani aliye ziumba mbingu na ardhi hawezi kuwaumba mfano wao? Kwani! Naye ndiye Muumbaji Mkuu, Mjuzi. |
| |
| 82 | Hakika amri yake anapo taka kitu ni kukiambia tu: Kuwa! Na kikawa. |
| |
| 83 | Basi Ametakasika yule ambaye mkononi mwake umo Ufalme wa kila kitu; na kwake Yeye mtarejeshwa. |
| |