37 - ASS'AFFAT |
| |
|
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU. |
| |
| |
| 1 | Naapa kwa wanao jipanga kwa safu. |
| |
| 2 | Na kwa wenye kukataza mabaya. |
| |
| 3 | Na kwa wenye kusoma Ukumbusho. |
| |
| 4 | Hakika Mungu wenu bila ya shaka ni Mmoja. |
| |
| 5 | Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, na yaliyomo kati yao, na ni Mola Mlezi wa mashariki zote. |
| |
| 6 | Hakika Sisi tumeipamba mbingu ya karibu kwa pambo la nyota. |
| |
| 7 | Na kulinda na kila shet'ani a'si. |
| |
| 8 | Wasiweze kuwasikiliza viumbe watukufu. Na wanafukuzwa huko kila upande. |
| |
| 9 | Wakifurushwa. Na wanayo adhabu ya kudumu. |
| |
| 10 | Isipo kuwa anaye nyakua kitu kidogo, na mara humfwatia kimondo kinacho ng'ara. |
| |
| 11 | Hebu waulize: Je! Wao ni wenye umbo gumu zaidi au hao wengine tulio waumba. Hakika Sisi tuliwaumba wao kwa udongo unao nata. |
| |
| 12 | Bali unastaajabu, na wao wanafanya maskhara. |
| |
| 13 | Na wanapo kumbushwa hawakumbuki. |
| |
| 14 | Na wanapo ona Ishara, wanafanya maskhara. |
| |
| 15 | Na husema: Haya si chochote ila ni uchawi tu ulio dhaahiri. |
| |
| 16 | Ati tukisha kufa na tukawa udongo na mifupa ndio kweli tutafufuliwa? |
| |
| 17 | Hata baba zetu wa zamani? |
| |
| 18 | Sema: Naam! Hali nanyi ni madhalili. |
| |
| 19 | Huko utapigwa ukelele mmoja tu! Na hapo ndio wataona! |
| |
| 20 | Watasema: Ole wetu! Hii ndiyo Siku ya Malipo. |
| |
| 21 | Hii ndiyo Siku ya Hukumu mliyo kuwa mkiikadhibisha. |
| |
| 22 | Wakusanyeni walio dhulumu, na wake zao, na hao walio kuwa wakiwaabudu - |
| |
| 23 | Badala ya Mwenyezi Mungu. Waongozeni njia ya Jahannamu! |
| |
| 24 | Na wasimamisheni. Hakika hao watasailiwa: |
| |
| 25 | Mna nini? Mbona hamsaidiani? |
| |
| 26 | Bali hii leo, watasalimu amri. |
| |
| 27 | Watakabiliana wao kwa wao kuulizana. |
| |
| 28 | Watasema: Kwa hakika nyinyi mlikuwa mkitujia upande wa kulia. |
| |
| 29 | Watasema (wakubwa): Bali nyinyi wenyewe hamkuwa Waumini. |
| |
| 30 | Sisi hatukuwa na mamlaka juu yenu, bali nyinyi wenyewe mlikuwa wapotovu. |
| |
| 31 | Basi hukumu ya Mola wetu Mlezi imekwisha tuthibitikia. Hakika bila ya shaka tutaonja tu adhabu. |
| |
| 32 | Tulikupotezeni kwa sababu sisi wenyewe tulikuwa wapotovu. |
| |
| 33 | Basi wao kwa hakika siku hiyo watashirikiana katika adhabu pamoja. |
| |
| 34 | Hivyo ndivyo tutakavyo wafanyia wakosefu. |
| |
| 35 | Wao walipo kuwa wakiambiwa La ilaha illa 'Llahu Hapana mungu ila Mwenyezi Mungu tu, wakijivuna. |
| |
| 36 | Na wakisema: Hivyo sisi tuiache miungu yetu kwa ajili ya huyu mtunga mashairi mwendawazimu? |
| |
| 37 | Bali huyu amekuja kwa Haki, na amewasadikisha Mitume. |
| |
| 38 | Hakika nyinyi bila ya shaka mtaionja adhabu chungu. |
| |
| 39 | Wala hamlipwi ila hayo mliyo kuwa mkiyafanya. |
| |
| 40 | Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio khitariwa. |
| |
| 41 | Hao ndio watakao pata riziki maalumu, |
| |
| 42 | Matunda, nao watahishimiwa. |
| |
| 43 | Katika Bustani za neema. |
| |
| 44 | Wako juu ya viti wamekabiliana. |
| |
| 45 | Wanazungushiwa kikombe chenye kinywaji cha chemchem |
| |
| 46 | Kinywaji cheupe, kitamu kwa wanywao. |
| |
| 47 | Hakina madhara, wala hakiwaleweshi. |
| |
| 48 | Na watakuwa nao wanawake wenye macho ya staha mazuri. |
| |
| 49 | Hao wanawake kama mayai yaliyo hifadhika. |
| |
| 50 | Waingie kuulizana wenyewe kwa wenyewe. |
| |
| 51 | Aseme msemaji mmoja miongoni mwao: Hakika mimi nalikuwa na rafiki |
| |
| 52 | Aliye kuwa akinambia: Hivyo wewe ni katika wanao sadiki |
| |
| 53 | Ati tukisha kufa tukawa udongo na mafupa, ndio tutalipwa na kuhisabiwa? |
| |
| 54 | Atasema: Je! Nyie mnawaona? |
| |
| 55 | Basi atachungulia amwone katikati ya Jahannamu. |
| |
| 56 | Atasema: Wallahi! Ulikaribia kunipoteza. |
| |
| 57 | Na lau kuwa si neema ya Mola wangu Mlezi bila ya shaka ningeli kuwa miongoni mwa walio hudhurishwa. |
| |
| 58 | Je! Sisi hatutakufa, |
| |
| 59 | Isipo kuwa kifo chetu cha kwanza? Wala sisi hatutaadhibiwa. |
| |
| 60 | Hakika huku bila ya shaka ndiko kufuzu kukubwa. |
| |
| 61 | Kwa mfano wa haya nawatende watendao. |
| |
| 62 | Je! Kukaribishwa hivi si ndio bora, au mti wa Zaqqum? |
| |
| 63 | Hakika Sisi tumeufanya huo kuwa ni mateso kwa walio dhulumu. |
| |
| 64 | Hakika huo ni mti unao toka katikati ya Jahannamu. |
| |
| 65 | Mashada ya matunda yake kama kwamba vichwa vya mashet'ani. |
| |
| 66 | Basi hakika bila ya shaka hao watayala hayo, na wajaze matumbo. |
| |
| 67 | Kisha juu yake wanyweshwe mchanganyo wa maji yamoto yaliyo chemka. |
| |
| 68 | Kisha hakika marejeo yao bila ya shaka yatakuwa kwenye Jahannamu. |
| |
| 69 | Hakika waliwakuta baba zao wamepotea. |
| |
| 70 | Na wao wakafanya haraka kufuata nyayo zao. |
| |
| 71 | Na bila ya shaka walikwisha potea kabla yao wengi wa watu wa zamani. |
| |
| 72 | Na Sisi hakika tuliwapelekea waonyaji. |
| |
| 73 | Basi hebu angalia ulikuwaje mwisho wa walio onywa. |
| |
| 74 | Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio khitariwa. |
| |
| 75 | Na hakika Nuhu alitwita, na Sisi ni bora wa waitikiaji. |
| |
| 76 | Na tulimwokoa yeye na ahali zake kutokana na msiba mkubwa. |
| |
| 77 | Na tuliwajaalia dhuriya zake ndio wenye kubakia. |
| |
| 78 | Na tukamwachia (sifa njema) kwa walio kuja baadaye. |
| |
| 79 | Iwe salama kwa Nuhu ulimwenguni kote! |
| |
| 80 | Kwa hakika hivi ndivyo tunavyo walipa wanao fanya mema. |
| |
| 81 | Hakika yeye ni katika waja wetu walio amini. |
| |
| 82 | Kisha tukawazamisha wale wengine. |
| |
| 83 | Na hakika Ibrahim alikuwa katika kundi lake, |
| |
| 84 | Alipo mjia Mola wake Mlezi kwa moyo mzima. |
| |
| 85 | Alimwambia baba yake na watu wake: Mnaabudu nini? |
| |
| 86 | Kwa kuzua tu mnataka miungu mingine badala ya Mwenyezi Mungu? |
| |
| 87 | Mnamdhania nini Mola Mlezi wa walimwengu wote? |
| |
| 88 | Kisha akapiga jicho kutazama nyota. |
| |
| 89 | Akasema: Hakika mimi ni mgonjwa! |
| |
| 90 | Nao wakamwacha, wakampa kisogo. |
| |
| 91 | Basi akaiendea miungu yao kwa siri, akaiambia: Mbona hamli? |
| |
| 92 | Mna nini hata hamsemi? |
| |
| 93 | Kisha akaigeukia kuipiga kwa mkono wa kulia. |
| |
| 94 | Basi wakamjia upesi upesi. |
| |
| 95 | Akasema: Hivyo mnaviabudu vitu mnavyo vichonga wenyewe? |
| |
| 96 | Na hali Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni nyinyi na hivyo mnavyo vifanya! |
| |
| 97 | Wakasema: Mjengeeni jengo, na kisha mtupeni motoni humo! |
| |
| 98 | Basi walitaka kumfanyia vitimbi, lakini tukawafanya wao ndio wa chini. |
| |
| 99 | Na akasema: Hakika mimi nahama, nakwenda kwa Mola wangu Mlezi; Yeye ataniongoa. |
| |
| 100 | Ewe Mola wangu Mlezi! Nitunukie aliye miongoni mwa watenda mema. |
| |
| 101 | Basi tukambashiria mwana aliye mpole. |
| |
| 102 | Basi alipo fika makamo ya kwenda na kurudi pamoja naye, alimwambia: Ewe mwanangu! Hakika mimi nimeona usingizini kuwa ninakuchinja. Basi angalia wewe, waonaje? Akasema: Ewe baba yangu! Tenda unavyo amrishwa, utanikuta mimi, Inshallah, katika wanao subiri. |
| |
| 103 | Basi wote wawili walipo jisalimisha, na akamlaza juu ya kipaji. |
| |
| 104 | Tulimwita: Ewe Ibrahim! |
| |
| 105 | Umekwisha itimiliza ndoto. Hakika hivi ndivyo tunavyo walipa wanao tenda mema. |
| |
| 106 | Hakika haya ni majaribio yaliyo dhaahiri. |
| |
| 107 | Basi tukamtolea fidia kwa dhabihu mtukufu. |
| |
| 108 | Na tukamwachia (sifa njema) kwa watu walio kuja baadaye. |
| |
| 109 | Iwe salama kwa Ibrahim! |
| |
| 110 | Hivi ndivyo tunavyo walipa wanao fanya mema. |
| |
| 111 | Hakika yeye ni katika waja wetu walio amini. |
| |
| 112 | Na tukambashiria kuzaliwa Is-haqa, naye ni Nabii miongoni mwa watu wema. |
| |
| 113 | Na tukambarikia yeye na Is-haqa. Na miongoni mwa dhuriya zao walitokea wema na wenye kudhulumu nafsi zao waziwazi. |
| |
| 114 | Na kwa hakika tuliwafanyia hisani Musa na Haruni. |
| |
| 115 | Na tukawaokoa wao na watu wao kutokana na dhiki kubwa. |
| |
| 116 | Na tukawanusuru; na wakawa wao ndio wenye kushinda. |
| |
| 117 | Na tukawapa wawili hao Kitabu kinacho bainisha. |
| |
| 118 | Na tukawaongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka. |
| |
| 119 | Na tukawaachia (sifa njema) katika watu walio kuja baadaye. |
| |
| 120 | Iwe salama kwa Musa na Haruni! |
| |
| 121 | Hakika hivyo ndivyo tunavyo walipa walio wema. |
| |
| 122 | Hakika wawili hao ni katika waja wetu walio amini. |
| |
| 123 | Na hakika Ilyas bila ya shaka alikuwa miongoni mwa Mitume. |
| |
| 124 | Alipo waambia watu wake: Hamwogopi? |
| |
| 125 | Mnamwomba Baa'li na mnamwacha Mbora wa waumbaji, |
| |
| 126 | Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wenu na Mola Mlezi wa baba zenu wa zamani? |
| |
| 127 | Wakamkadhibisha. Basi kwa hakika watahudhurishwa; |
| |
| 128 | Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio safishwa. |
| |
| 129 | Na tumemwachia (sifa nzuri) kwa walio kuja baadaye. |
| |
| 130 | Iwe salama kwa Ilyas. |
| |
| 131 | Hakika hivyo ndivyo tunavyo walipa walio wema. |
| |
| 132 | Hakika yeye ni katika waja wetu walio amini. |
| |
| 133 | Na hakika Lut'i bila ya shaka ni miongoni mwa Mitume. |
| |
| 134 | Tulipo mwokoa yeye na ahali zake wote, |
| |
| 135 | Isipo kuwa mwanamke mkongwe katika wale walio bakia nyuma. |
| |
| 136 | Kisha tukawaangamiza wale wengineo. |
| |
| 137 | Na hakika nyinyi mnawapitia wakati wa asubuhi, |
| |
| 138 | Na usiku. Basi je! Hamyatii akilini? |
| |
| 139 | Na hakika Yunus alikuwa miongoni mwa Mitume. |
| |
| 140 | Alipo kimbia katika jahazi lilio sheheni. |
| |
| 141 | Akaingia katika kupigiwa kura, na akawa katika walio shindwa. |
| |
| 142 | Samaki akammeza hali ya kuwa ni mwenye kulaumiwa. |
| |
| 143 | Na ingeli kuwa hakuwa katika wanao mtakasa Mwenyezi Mungu, |
| |
| 144 | Bila ya shaka angeli kaa ndani yake mpaka siku ya kufufuliwa. |
| |
| 145 | Lakini tulimtupa ufukweni patupu, hali yu mgonjwa. |
| |
| 146 | Na tukauotesha juu yake mmea wa kabila ya mung'unye. |
| |
| 147 | Na tulimtuma kwa watu laki moja au zaidi. |
| |
| 148 | Basi wakaamini, na tukawastarehesha kwa muda. |
| |
| 149 | Basi waulize: Ati Mola wako Mlezi ndiye mwenye watoto wa kike, na wao wanao watoto wa kiume? |
| |
| 150 | Au tumewaumba Malaika kuwa ni wanawake, na wao wakashuhudia? |
| |
| 151 | Ati ni kwa uzushi wao ndio wanasema: |
| |
| 152 | Mwenyezi Mungu amezaa! Ama hakika bila ya shaka hao ni waongo! |
| |
| 153 | Ati amekhiari watoto wa kike kuliko wanaume? |
| |
| 154 | Mna nini? Mnahukumu vipi nyinyi? |
| |
| 155 | Hamkumbuki? |
| |
| 156 | Au mnayo hoja iliyo wazi? |
| |
| 157 | Basi leteni Kitabu chenu kama mnasema kweli. |
| |
| 158 | Na wameweka makhusiano ya nasaba baina yake na majini; na majini wamekwisha jua bila ya shaka kuwa wao watahudhurishwa. |
| |
| 159 | Subhana 'Llah Ametakasika Mwenyezi Mungu na hayo wanayo msingizia. |
| |
| 160 | Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio safishwa. |
| |
| 161 | Basi hakika nyinyi na mnao waabudu |
| |
| 162 | Hamwezi kuwapoteza |
| |
| 163 | Isipo kuwa yule atakaye ingia Motoni. |
| |
| 164 | Na hapana katika sisi ila anapo mahali pake maalumu. |
| |
| 165 | Na hakika bila ya shaka sisi ndio wajipangao safu. |
| |
| 166 | Na hakika sisi ndio wenye kusabihi kutakasa. |
| |
| 167 | Na walikuwapo walio kuwa wakisema: |
| |
| 168 | Tungeli kuwa na Ukumbusho kama wa watu wa zamani, |
| |
| 169 | Bila ya shaka tungeli kuwa ni waja wa Mwenyezi Mungu wenye ikhlasi. |
| |
| 170 | Lakini waliukataa. Basi watakuja jua. |
| |
| 171 | Na bila ya shaka neno letu lilikwisha tangulia kwa waja wetu walio tumwa. |
| |
| 172 | Ya kuwa wao bila ya shaka ndio watakao nusuriwa. |
| |
| 173 | Na kwamba jeshi letu ndilo litakalo shinda. |
| |
| 174 | Basi waachilie mbali kwa muda. |
| |
| 175 | Na watazame, nao wataona. |
| |
| 176 | Je! Wanaihimiza adhabu yetu? |
| |
| 177 | Basi itakapo shuka uwanjani kwao, itakuwa asubuhi mbaya kwa walio onywa. |
| |
| 178 | Na waache kwa muda. |
| |
| 179 | Na tazama, na wao wataona. |
| |
| 180 | Subhana Rabbi'l'Izzat Ametakasika Mola Mlezi Mwenye enzi na yale wanayo mzulia. |
| |
| 181 | Na Salamu juu ya Mitume. |
| |
| 182 | Na sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote. |
| |