51 - ADH-DHAARIYAAT |
| |
|
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU. |
| |
| |
| 1 | Naapa kwa pepo zinazo tawanya, |
| |
| 2 | Na zinazo beba mizigo, |
| |
| 3 | Na zinazo kwenda kwa wepesi. |
| |
| 4 | Na zinazo gawanya kwa amri, |
| |
| 5 | Hakika mnayo ahidiwa bila ya shaka ni kweli, |
| |
| 6 | Na kwa hakika malipo bila ya shaka yatatokea. |
| |
| 7 | Naapa kwa mbingu zenye njia, |
| |
| 8 | Hakika nyinyi bila ya shaka mmo katika kauli inayo khitalifiana. |
| |
| 9 | Anageuzwa kutokana na haki mwenye kugeuzwa. |
| |
| 10 | Wazushi wameangamizwa. |
| |
| 11 | Ambao wameghafilika katika ujinga. |
| |
| 12 | Wanauliza: Ni lini hiyo siku ya malipo? |
| |
| 13 | Hiyo ni siku watakayo adhibiwa Motoni. |
| |
| 14 | Onjeni adhabu yenu! Haya ndiyo mliyo kuwa mkiyahimiza. |
| |
| 15 | Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na chemchem. |
| |
| 16 | Wanapokea aliyo wapa Mola wao Mlezi. Kwa hakika hao walikuwa kabla ya haya wakifanya mema. |
| |
| 17 | Walikuwa wakilala kidogo tu usiku. |
| |
| 18 | Na kabla ya alfajiri wakiomba maghfira. |
| |
| 19 | Na katika mali yao ipo haki ya mwenye kuomba na asiye omba. |
| |
| 20 | Na katika ardhi zipo Ishara kwa wenye yakini. |
| |
| 21 | Na pia katika nafsi zenu - Je! Hamwoni? |
| |
| 22 | Na katika mbingu ziko riziki zenu na mliyo ahidiwa. |
| |
| 23 | Basi naapa kwa Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, hakika haya ni kweli kama ilivyo kweli kuwa nyinyi mnasema. |
| |
| 24 | Je! Imekufikia hadithi ya wageni wa Ibrahim wanao hishimiwa? |
| |
| 25 | Walipo ingia kwake wakasema: Salama! Na yeye akasema: Salama! Nyinyi ni watu nisio kujueni. |
| |
| 26 | Akenda kwa ahali yake na akaja na ndama aliye nona. |
| |
| 27 | Akawakaribisha, akasema: Mbona hamli? |
| |
| 28 | Akahisi kuwaogopa katika nafsi yake. Wakasema: Usiwe na khofu, nao wakambashiria kupata kijana mwenye ilimu. |
| |
| 29 | Ndipo mkewe akawaelekea, na huku anasema na akijipiga usoni kwa mastaajabu, na kusema: Mimi ni kikongwe na tasa! |
| |
| 30 | Wakasema: Ndivyo vivyo hivyo alivyo sema Mola wako Mlezi. Hakika Yeye ni Mwenye hikima na Mwenye kujua. |
| |
| 31 | AKASEMA: Basi ujumbe wenu ni nini, enyi mlio tumwa? |
| |
| 32 | Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwa watu wakosefu, |
| |
| 33 | Tuwatupie mawe ya udongo, |
| |
| 34 | Yaliyo tiwa alama kutoka kwa Mola wako Mlezi kwa ajili ya wanao pindukia mipaka. |
| |
| 35 | Kwa hivyo tutawatoa katika hao wale walio amini. |
| |
| 36 | Lakini hatukupata humo ila nyumba moja tu yenye Waislamu! |
| |
| 37 | Na tukaacha humo Ishara kwa ajili ya wanao iogopa adhabu chungu. |
| |
| 38 | Na katika khabari za Musa, tulipo mtuma kwa Firauni na hoja wazi. |
| |
| 39 | Lakini alipuuza kwa sababu ya nguvu zake na akasema: Huyu ni mchawi au mwendawazimu! |
| |
| 40 | Basi tukamkamata yeye na majeshi yake na tukawatupa baharini, na yeye ndiye wa kulaumiwa. |
| |
| 41 | Na katika khabari za A'di tulipo wapelekea upepo wa kukata uzazi. |
| |
| 42 | Haukuacha chochote ulicho kifikia ila ulikifanya kama kilio nyambuka. |
| |
| 43 | Na katika khabari za Thamudi walipo ambiwa: Jifurahisheni kwa muda mdogo tu. |
| |
| 44 | Wakaasi amri ya Mola wao Mlezi. Basi uliwanyakua moto wa radi nao wanaona. |
| |
| 45 | Basi hawakuweza kusimama wala hawakuwa wenye kujitetea. |
| |
| 46 | Na kaumu ya Nuhu hapo mbele. Hakika hao walikuwa watu wapotovu. |
| |
| 47 | Na mbingu tumezifanya kwa nguvu na uwezo na hakika Sisi bila ya shaka ndio twenye uwezo wa kuzitanua. |
| |
| 48 | Na ardhi tumeitandaza; basi watandazaji wazuri namna gani Sisi! |
| |
| 49 | Na katika kila kitu tumeumba kwa jozi ili mzingatie. |
| |
| 50 | Basi kimbilieni kwa Mwenyezi Mungu, hakika mimi ni mwonyaji kwenu wa kubainisha nitokae kwake. |
| |
| 51 | Wala msifanye kuwa kuna mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu. Hakika mimi ni mwonyaji kwenu wa kubainisha nitokae kwake. |
| |
| 52 | Basi ndio hivyo hivyo, hakuwajia kabla yao Mtume ila walisema: Huyu ni mchawi au mwendawazimu. |
| |
| 53 | Je! Wameambizana kwa haya? Bali hawa ni watu waasi. |
| |
| 54 | Basi waachilie mbali, nawe hulaumiwi. |
| |
| 55 | Na kumbusha, kwani ukumbusho huwafaa Waumini. |
| |
| 56 | Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi. |
| |
| 57 | Na sitaki kwao riziki, wala sitaki wanilishe. |
| |
| 58 | Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuruzuku, Mwenye nguvu, Madhubuti. |
| |
| 59 | Hakika walio dhulumu wana fungu lao la adhabu kama fungu la wenzao. Basi wasinihimize. |
| |
| 60 | Ole wao walio ikanusha siku yao waliyo ahidiwa. |
| |