___Translations___

_Quran?_

_Gadgets_

_Search_

_Links_

_Contribute_

_Note_

1 - AL-FAATIH'A
2 - AL - BAQARA
3 - AL I'MRAN
4 - AN-NISAAI
5 - AL - MAIDA
6 - AL - AN-A'AM
7 - AL - A'RAAF
8 - AL - ANFAAL
9 - AT-TAWBA
10 - YUNUS
11 - HUD
12 - YUSUF
13 - AR-RAA'D
14 - IBRAHIM
15 - AL - HIJR
16 - AN NAH'L
17 - AL ISRAAI (BANI ISRAIL)
18 - AL - KAHF
19 - MARYAM
20 - T'AHA
21 - AL - ANBIYAA
22 - AL -HAJJ
23 - AL - MUUMINUN
24 - AN - NUR
25 - AL - FURQAN
26 - ASH-SHUA'RAA
27 - AN-NAML
28 - AL-QAS'AS'
29 - AL - A'NKABUT
30 - AR-RUM
31 - LUQMAN
32 - ASSAJDAH
33 - AL-AH'ZAB
34 - SABAA
35 - FAAT'IR
36 - YA-SIN
37 - ASS'AFFAT
38 - S'AAD
39 - AZZUMAR
40 - GHAAFIR (AU AL MUUMIN)
41 - FUSS'ILAT (AU H'A MIM SAJDAH)
42 - ASH-SHUURA
43 - AZZUKHRUF
44 - ADDUKHAN
45 - AL - JAATHIYA
46 - AL - AH'QAAF
47 - MUH'AMMAD
48 - AL FAT-H'I
49 - AL H'UJURAAT
50 - QAAF
51 - ADH-DHAARIYAAT
52 - ATT'UR
53 - ANNAJM
54 - AL-QAMAR
55 - ARRAH'MAN
56 - AL -WAAQIA'H
57 - AL -H'ADIID
58 - AL - MUJAADALAH
59 - AL - H'ASHRI
60 - AL - MUMTAH'INAH
61 - ASS'AF
62 - AL - JUMUA'
63 - AL - MUNAAFIQUN
64 - ATTAGHAABUN
65 - ATT'ALAAQ
66 - ATTAH'RIIM
67 - AL - MULK
68 - AL - QALAM
69 - AL - H'AAQQAH
70 - AL - MAA'RIJ
71 - NUH'
72 - AL - JINN
73 - AL - MUZZAMMIL
74 - AL - MUDDATHTHIR
75 - AL - QIYAMAH
76 - AL - INSAN
77 - AL - MURSALAAT
78 - ANNABAA
79 - ANNAZIA'AT
80 - A'BASA
81 - ATTAKWIR
82 - AL - INFIT'AAR
83 - AL - MUT'AFFIFIIN
84 - AL - INSHIQAAQ
85 - AL - BURUUJ
86 - ATT'AARIQ
87 - AL - AA'LAA
88 - AL - GHAASHIYAH
89 - AL - FAJR
90 - AL - BALAD
91 - ASH-SHAMS
92 - AL - LAYL
93 - WADH-DHUH'AA
94 - ASH-SHARH'
95 - AT-TIN
96 - AL - A'LAQ
97 - AL - QADR
98 - AL - BAYYINAH
99 - AZ-ZILZALAH
100 - AL - A'ADIYAAT
101 - AL - QAARIA'H
102 - AT-TAKAATHUR
103 - AL - A'S'R
104 - AL - HUMAZAH
105 - AL - FIIL
106 - QURAISH
107 - AL - MAAU'N
108 - AL - KAWTHAR
109 - AL - KAFIRUN
110 - ANNAS'R
111 - AL - MASAD
112 - AL - IKHLAS'
113 - AL - FALAQ
114 - ANNAS
KISWAHILI

11 - HUD

 

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.

 
1Alif Lam Ra. Hiki ni Kitabu ambacho Aya zake zimewekwa wazi, kisha zikapambanuliwa, kilicho toka kwa Mwenye Hikima na Mwenye Khabari,
 
2Ili msimuabudu isipo kuwa Allah, Mwenyezi Mungu. Hakika mimi kwenu ni mwonyaji na mbashiri nitokae kwake.
 
3Na ili mumwombe msamaha Mola wenu Mlezi, kisha mtubie kwake. Atakustarehesheni starehe nzuri mpaka muda maalumu. Na atampa kila mwenye fadhila, fadhila yake. Na ikiwa mtakengeuka basi mimi nakukhofieni adhabu ya hiyo Siku Kubwa.
 
4Marejeo yenu ni kwa Mwenyezi Mungu tu. Naye ni Muweza wa kila kitu.
 
5Hebu angalia! Ati wanafunika vilivyomo vifuani mwao ili wamfiche Mwenyezi Mungu! Jueni kuwa wanapo jigubika nguo zao Yeye anajua wanayo yaficha na wanayo yatangaza. Hakika Yeye ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani.
 
6NA HAKUNA mnyama yoyote katika ardhi ila riziki yake iko kwa Mwenyezi Mungu. Naye anajua makao yake na mapitio yake. Yote yamo katika Kitabu chenye kubainisha.
 
7Na Yeye ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi katika siku sita. Na Kiti chake cha Enzi kilikuwa juu ya maji, ili akufanyieni mtihani ajuulikane ni nani miongoni mwenu mzuri zaidi wa vitendo. Na wewe ukisema: Nyinyi hakika mtafufuliwa baada ya kufa; wale walio kufuru husema: Hayakuwa haya ila ni uchawi uliyo wazi.
 
8Na tukiwacheleweshea adhabu mpaka muda ulio kwisha hisabiwa wao husema: Nini kinacho izuia hiyo adhabu? Jueni! Siku itakapo wajia basi haitoondolewa hiyo kwao. Na yatawazunguka yale waliyo kuwa wakiyafanyia mzaha.
 
9Na tukimwonjesha mtu rehema inayo toka kwetu, kisha tukamwondolea, hukata tamaa akakufuru.
 
10Na tukimwonjesha neema baada ya madhara yaliyo mpata husema: Taabu zimekwisha niondokea. Hakika yeye hujitapa na kutafakhari.
 
11Ila wale walio subiri wakatenda mema. Hao watapata msamaha na ujira mkubwa.
 
12Basi labda utaacha baadhi ya yale yaliyo funuliwa kwako, na kifua kitaona dhiki kwa hayo, kwa sababu wanasema: Mbona hakuteremshiwa khazina, au wakaja naye Malaika? Wewe ni mwonyaji tu, na Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wa kila kitu.
 
13Au wanasema: Ameizua? Sema: Basi leteni Sura kumi zilizo zuliwa mfano wa hii, na waiteni muwawezao badala ya Mwenyezi Mungu, ikiwa mnasema kweli.
 
14Na wasipo kuitikieni, basi jueni ya kwamba (hii Qur'ani) imeteremshwa kwa ujuzi wa Mwenyezi Mungu, na kwamba hapana mungu ila Yeye. Basi je! Nyinyi ni Waislamu?
 
15Wanao taka maisha ya dunia na pumbao lake tutawalipa humo vitendo vyao kaamili. Na wao humo hawatopunjwa.
 
16Hao ndio ambao hawatakuwa na kitu Akhera ila Moto, na yataharibika waliyo yafanya, na yatapotea bure waliyo kuwa wakiyatenda.
 
17Basi je, mtu aliye na dalili wazi itokayo kwa Mola wake Mlezi, inayo fuatwa na shahidi anaye toka kwake, na kabla yake kilikuwa Kitabu cha Musa kilicho kuwa mwongozi na rehema - hao wanamuamini, na anaye mkataa katika makundi, basi Moto ndio pahala pa miadi yao. Basi usiwe na shaka juu ya hayo. Hii ni Haki itokayo kwa Mola wako Mlezi; lakini watu wengi hawaamini.
 
18Na nani aliye dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye mzulia Mwenyezi Mungu uwongo? Hao watahudhurishwa mbele ya Mola wao Mlezi, na mashahidi watasema: Hawa ndio walio mtungia uwongo Mola wao Mlezi. Laana ya Mwenyezi Mungu iwapate walio dhulumu,
 
19Ambao wanazuilia Njia ya Mwenyezi Mungu, na wanaitakia ipotoke, na wanaikataa Akhera.
 
20Hao hawawezi kushinda katika ardhi, wala hawana walinzi isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Watazidishiwa adhabu. Hawakuwa wakiweza kusikia wala hawakuwa wakiona.
 
21Hao ndio walio zikhasiri nafsi zao, na yakawapotea waliyo kuwa wakiyazua.
 
22Bila ya shaka hakika wao ndio wenye kukhasiri huko Akhera.
 
23Hakika wale walio amini,na wakatenda mema, na wakanyenyekea kwa Mola wao Mlezi, hao ndio watu wa Peponi, na humo watadumu.
 
24Mfano wa makundi mawili ni kama kipofu kiziwi, na mwenye kuona na anasikia. Je, wawili hawa wanakuwa sawa kwa kufananishwa? Basi, je, hamfikiri?
 
25Na Sisi tulimtuma Nuhu kwa watu wake, akawaambia: Hakika mimi ni mwonyaji kwenu ninaye bainisha,
 
26Ya kwamba msimuabudu isipo kuwa Mwenyezi Mungu tu. Hakika mimi ninakukhofieni adhabu ya Siku Chungu.
 
27Na wakasema wakuu walio kufuru katika kaumu yake: Hatukuoni wewe ila ni mtu tu kama sisi, wala hatukuoni wamekufuata ila wale walio kuwa kwetu watu duni, wasio kuwa na akili. Wala hatukuoneni kuwa mna ubora wowote kutushinda sisi. Bali tuna hakika nyinyi ni waongo.
 
28Akasema: Enyi watu wangu! Hebu fikirini! Ikiwa mimi ninayo hoja wazi iliyo toka kwa Mola wangu Mlezi, na amenipa rehema kutoka kwake, nayo ikakufichikieni; je, tukulazimisheni kuikubali hali nyinyi mnaichukia?
 
29Na enyi watu wangu! Mimi sikuombeni mali kwa ajili ya haya. Mimi sina ujira ila kwa Mwenyezi Mungu; na mimi sitawafukuza walio amini. Hakika wao watakutana na Mola wao Mlezi, lakini mimi nakuoneni mnafanya ujinga.
 
30Na enyi watu wangu! Ni nani atakaye nisaidia kwa Mwenyezi Mungu nikiwafukuza hawa? Basi je, hamfikiri?
 
31Wala sikwambiini kuwa nina khazina za Mwenyezi Mungu; wala kuwa mimi najua mambo ya ghaibu; wala sisemi: Mimi ni Malaika. Wala siwasemi wale ambao yanawadharau macho yenu kuwa Mwenyezi Mungu hatawapa kheri - Mwenyezi Mungu anajua yaliomo katika nafsi zao - hapo bila ya shaka ninge kuwa miongoni mwa wenye kudhulumu.
 
32Wakasema: Ewe Nuhu! Umejadiliana, na umekithirisha kutujadili. Basi tuletee hayo unayo tuahidi, ukiwa miongoni mwa wasemao kweli.
 
33Akasema: Mwenyezi Mungu atakuleteeni akipenda. Wala nyinyi si wenye kumshinda.
 
34Wala nasaha yangu haikufaini kitu nikitaka kukunasihini, ikiwa Mwenyezi Mungu anataka kukuachieni mpotee. Yeye ndiye Mola wenu Mlezi; na kwake mtarejeshwa.
 
35Au ndio wanasema: Ameizua? Sema: Ikiwa nimeizua, basi kosa hilo ni juu yangu, na mimi sikhusiki na makosa myatendayo.
 
36Na akafunuliwa Nuhu akaambiwa: Hataamini yeyote katika watu wako ila wale walio kwisha amini. Basi usisikitike kwa waliyo kuwa wakiyatenda.
 
37Na unda jahazi mbele ya macho yetu na kwa mujibu wa ufunuo wetu. Wala usinisemeze kuwatetea walio dhulumu. Kwani hao bila ya shaka watazamishwa.
 
38Na akawa anaunda jahazi, na kila wakipita wakuu wa kaumu yake wakimkejeli. Yeye akasema: Ikiwa nyinyi mnatukejeli na sisi tunakukejelini kama mnavyo tukejeli.
 
39Nanyi mtakuja jua ni nani itakaye mfikia adhabu ya kumhizi, na itakaye mteremkia adhabu ya kudumu.
 
40Hata ilipo kuja amri yetu, na tanuri ikafoka maji, tulisema: Pakia humo wawili wawili, dume na jike, kutoka kila aina, na ahali zako, isipo kuwa wale ambao imekwisha wapitia hukumu; na watu walio amini. Na hawakuamini pamoja naye ila wachache tu.
 
41Na akasema: Pandeni humo kwa Bismillahi, Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, kwenda kwake na kusimama kwake. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
 
42Ikawa inakwenda nao katika mawimbi kama milima. Na Nuhu akamwita mwanawe naye alikuwa mbali: Ewe mwanangu! Panda pamoja nasi, wala usiwe pamoja na makafiri.
 
43Akasema: Nitakimbilia mlimani unilinde na maji. (Nuhu) akasema: Leo hapana wa kulindwa na amri ya Mwenyezi Mungu ila aliye mrehemu mwenyewe. Na wimbi likawatenganisha, akawa katika walio zama.
 
44Na ikasemwa: Ewe ardhi! Meza maji yako. Na Ewe mbingu! Jizuie. Basi maji yakadidimia chini, na amri ikapitishwa, na (jahazi) likasimama juu ya (mlima) wa Al Juudiy. Na ikasemwa: Wapotelee mbali watu walio dhulumu!
 
45Na Nuhu alimwomba Mola wake Mlezi: Ee Mola Mlezi wangu! Hakika mwanangu ni katika ahali zangu, na hakika ahadi yako ni haki. Na Wewe ni Mwenye haki kuliko mahakimu wote.
 
46Akasema: Ewe Nuhu! Huyu si katika ahali zako. Mwendo wake si mwema. Basi usiniombe jambo usio na ujuzi nalo. Mimi nakuwaidhi usije ukawa miongoni mwa wajinga.
 
47Nuhu akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Mimi najikinga kwako nisikuombe nisio na ujuzi nalo. Na kama hunisamehe na ukanirehemu, nitakuwa katika walio khasiri.
 
48Ikasemwa: Ewe Nuhu! Shuka kwa salama itokayo kwetu, na baraka nyingi juu yako na juu ya watu walio pamoja nawe. Na zitakuwapo kaumu tutakazo zistarehesha, na kisha zitashikwa na adhabu chungu itokayo kwetu.
 
49Hizi ni katika khabari za ghaibu tunazo kufunulia. Hukuwa ukizijua wewe, wala watu wako, kabla ya hii. Basi subiri! Hakika Mwisho ni wa wachamngu.
 
50Na kwa kina A'adi tulimtuma ndugu yao Hud. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu! Nyinyi hamna mungu isipo kuwa Yeye. Nyinyi si chochote ila ni wazushi tu.
 
51Enyi watu wangu! Sikuombeni ujira kwa ajili ya haya. Haukuwa ujira wangu ila kwa Yule aliye niumba. Basi hamtumii akili?
 
52Na enyi watu wangu! Muombeni msamaha Mola wenu Mlezi, kisha mtubie kwake. Atakuleteeni mbingu zenye kunyesha mvua ya kumiminika, na atakuzidishieni nguvu juu ya nguvu zenu. Wala msigeuke mkawa wakosefu.
 
53Wakasema: Ewe Hud! Hujatuletea dalili wazi. Wala sisi hatuiachi miungu yetu kwa kufuata kauli yako. Na wala sisi hatukuamini wewe.
 
54Sisi tunasema: Baadhi katika miungu yetu imekusibu kwa baa. Akasema: Hakika mimi namshuhudisha Mwenyezi Mungu, na nyinyi shuhudieni, ya kwamba mimi najitenga mbali na hao mnao wafanya washirika,
 
55Mkamwacha Yeye. Basi nyote nyinyi nipangieni vitimbi, na kisha msinipe muhula!
 
56Hakika mimi nimemtegemea Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wangu na Mola Mlezi wenu. Hapana kiumbe yeyote ila Yeye anamwendesha atakavyo. Hakika Mola wangu Mlezi yuko juu ya Njia Iliyo Nyooka.
 
57Na ikiwa watarudi nyuma, basi mimi nimekwisha kufikishieni niliyo tumwa kwenu. Na Mola wangu Mlezi atawaleta watu wengine badala yenu, wala nyinyi hamumdhuru kitu Yeye. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mwenye kuhifadhi kila kitu.
 
58Ilipo fika amri yetu, tulimwokoa Hud na walio amini pamoja naye, kwa rehema itokayo kwetu. Na tukawaokoa na adhabu ngumu.
 
59Na hao ndio kina A'adi. Walizikanusha Ishara za Mola wao Mlezi, na wakawaasi Mitume wake, na wakafuata amri ya kila jabari mwenye inda.
 
60Na wakafuatishiwa laana katika dunia hii na Siku ya Kiyama. Basi tambueni mtanabahi! Hakika kina A'adi walimkufuru Mola wao Mlezi. Na tambueni mtanabahi kuwa hakika waliangamizwa kina A'adi, kaumu ya Hud.
 
61Na kina Thamud tuliwapelekea ndugu yao Saleh. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila Yeye. Yeye ndiye aliye kuumbeni katika ardhi, na akakuwekeni humo. Basi mwombeni msamaha, kisha mtubu kwake. Hakika Mola wangu Mlezi yupo karibu, anaitikia maombi.
 
62Wakasema: Ewe Saleh! Hakika kabla ya haya ulikuwa unatarajiwa kheri kwetu. Je, unatukataza tusiwaabudu waliyo kuwa wakiwaabudu baba zetu? Na hakika sisi tuna shaka na wasiwasi kwa hayo unayo tuitia.
 
63Akasema: Enyi watu wangu! Mwaonaje ikiwa ninazo dalili zilizo wazi kutokana na Mola wangu Mlezi, naye akawa kanipa rehema kutoka kwake - je, ni nani atakaye ninusuru kwa Mwenyezi Mungu nikimuasi? Basi nyinyi hamtanizidishia ila khasara tu.
 
64Enyi watu wangu! Huyu ngamia wa Mwenyezi Mungu ni Ishara kwenu. Basi mwacheni ale katika ardhi ya Mwenyezi Mungu; wala msimguse kwa ubaya, isije ikakuangamizeni adhabu iliyo karibu.
 
65Wakamchinja. Basi (Saleh) akasema: Stareheni katika mji wenu muda wa siku tatu. Hiyo ni ahadi isiyo kuwa ya uwongo.
 
66Basi ilipo kuja amri yetu tulimwokoa Saleh na wale walio amini pamoja naye kwa rehema yetu kutokana na hizaya ya siku ile. Hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kushinda.
 
67Na ukelele uliwaangamiza wale walio dhulumu, wakapambazukiwa nao ni maiti majumbani mwao.
 
68Kama kwamba hawakuwako huko. Hebu zingatieni! Hakika kina Thamud walimkufuru Mola wao Mlezi. Hebu zingatieni! Thamud wamepotelea mbali!
 
69Na wajumbe wetu walimjia Ibrahim kwa bishara njema, wakasema: Salama! Naye akasema: Salama! Hakukaa ila mara akaleta ndama wa kuchoma.
 
70Basi alipoona mikono yao haimfikilii aliwatilia shaka, na akawaogopa. Wakasema: Usiogope! Hakika sisi tumetumwa kwa kaumu ya Lut'.
 
71Na mkewe alikuwa kasimama wima, akacheka. Basi tukambashiria (kuzaliwa) Is-haq, na baada ya Is-haq Yaaqub.
 
72Akasema: Je, hivyo mimi nizae, na hali yangu ni kikongwe na huyu mume wangu ni kizee? Hakika haya ni mambo ya ajabu!
 
73Wakasema: Je, unastaajabia amri ya Mwenyezi Mungu? Rehema ya Mwenyezi Mungu na baraka zake ziko juu yenu, enyi watu wa nyumba hii! Hakika Yeye ndiye Msifiwa wa kutukuzwa.
 
74Basi khofu ilipo mwondoka Ibrahim, na ikawa ile bishara imemfikia, alianza kujadiliana nasi juu ya kaumu ya Lut'.
 
75Hakika Ibrahim alikuwa mpole, ana huruma, na mwepesi wa kurejea kwa Mwenyezi Mungu.
 
76(Akaambiwa): Ewe Ibrahim! Wachilia mbali haya! Kwa hakika amri ya Mola wako Mlezi imekwisha kuja, na hakika hao itawafikia adhabu isiyo rudi nyuma.
 
77Na wajumbe wetu walipo kuja kwa Lut' aliwahuzunukia na akawaonea dhiki. Akasema: Hii leo ni siku ngumu!
 
78Wakamjia kaumu yake mbio mbio. Na kabla ya haya walikuwa wakitenda maovu. Yeye akasema: Enyi watu wangu! Hawa binti zangu, ndio wametakasika zaidi kwenu. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, wala msinihizi mbele ya wageni wangu. Hivyo, hamna hata mtu mmoja miongoni mwenu aliye ongoka?
 
79Wakasema: Bila shaka umekwisha jua hatuna haki juu ya binti zako, na unayajua tunayo yataka.
 
80Akasema: Laiti ningeli kuwa na nguvu kwenu, au nategemea kwenye nguzo yenye nguvu!
 
81(Wajumbe) wakasema: Ewe Lut'! Sisi ni wajumbe wa Mola wako Mlezi. Hawa hawatakufikia. Na wewe ondoka pamoja na ahali zako usiku ungalipo. Wala yeyote miongoni mwenu asitazame nyuma, isipo kuwa mkeo, kwani yeye utamfika msiba utakao wafika hao. Hakika miadi yao ni asubuhi. Je, asubuhi si karibu?
 
82Basi ilipo fika amri yetu tuliigeuza nchi juu chini, na tukawateremshia mvua ya changarawe za udongo mgumu ulio kamatana wa Motoni,
 
83Zilizo tiwa alama kwa Mola wako Mlezi. Na haya hayako mbali na wenye kudhulumu wengineo.
 
84Na kwa watu wa Madyana tuliwatumia ndugu yao Shua'ib. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila Yeye, wala msipunguze vipimo na mizani. Mimi nakuoneni mmo katika hali njema, nami nakukhofieni adhabu ya Siku kubwa hiyo itakayo kuzungukeni.
 
85Na enyi watu wangu! Timizeni vipimo na mizani kwa uadilifu wala msiwakhini watu vitu vyao; wala msieneze uovu katika nchi mkafanya uharibifu.
 
86Alivyo kubakishieni Mwenyezi Mungu ndiyo bora kwa ajili yenu, ikiwa nyinyi ni Waumini. Wala mimi siye mlinzi wenu.
 
87Wakasema: Ewe Shua'ibu! Ni sala zako ndizo zinazo kuamrisha tuyaache waliyo kuwa wakiyaabudu baba zetu, au tuache kufanya tupendavyo katika mali zetu? Ama hakika wewe ni mstahamilivu kweli na mwongofu!
 
88Akasema: Enyi watu wangu! Mwaonaje ikiwa ninayo dalili wazi inayo tokana na Mola wangu Mlezi, na ikawa Yeye ameniruzuku riziki njema kutoka kwake? Wala mimi sipendi kukukhalifuni nikafanya yale ninayo kukatazeni. Sitaki ila kutengeneza kiasi ninavyo weza. Na sipati kuwezeshwa haya ila na Mwenyezi Mungu. Kwake Yeye ninategemea, na kwake Yeye naelekea.
 
89Na enyi watu wangu! Kukhalifiana nami kusikupelekeeni hata mkasibiwa kama walivyo sibiwa watu wa Nuhu, au watu wa Hud, au watu wa Saleh. Na watu wa Lut' si mbali nanyi.
 
90Na ombeni msamaha kwa Mola wenu Mlezi, tena tubuni kwake. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mwenye kurehemu na Mwenye upendo.
 
91Wakasema: Ewe Shua'ibu! Mengi katika hayo unayo yasema hatuyafahamu. Na sisi tunakuona huna nguvu kwetu. Lau kuwa si jamaa zako tunge kupiga mawe, wala wewe si mtukufu kwetu.
 
92Akasema: Enyi watu wangu! Kwani jamaa zangu ni watukufu zaidi kwenu kuliko Mwenyezi Mungu? Na Yeye mmemueka nyuma ya migongo yenu! Hakika Mola wangu Mlezi ni Mwenye kuyazunguka yote mnayo yatenda.
 
93Na enyi watu wangu! Fanyeni mwezayo, na mimi pia ninafanya. Karibuni mtajua ni nani itakaye mfikia adhabu ya kumhizi, na nani aliye mwongo. Na ngojeni, mimi pia ninangoja pamoja nanyi.
 
94Na ilipo fika amri yetu, tulimwokoa Shua'ibu na wale walio amini pamoja naye kwa rehema yetu. Na ukelele uliwanyakua walio dhulumu, na wakapambaukiwa majumbani mwao wamekufa kifudifudi!
 
95Kama kwamba hawakuwamo humo. Zingatia walivyo angamia watu wa Madyana, kama walivyo angamia watu wa Thamud!
 
96Na hakika tulimtuma Musa pamoja na Ishara zetu na uthibitisho ulio wazi
 
97Kwa Firauni na waheshimiwa wake. Lakini wao walifuata amri ya Firauni, na amri ya Firauni haikuwa yenye uwongofu.
 
98Siku ya Kiyama atawatangulia watu wake na atawaingiza Motoni. Na muingio muovu ulioje huo!
 
99Nao wamefuatishiwa laana hapa duniani na Siku ya Kiyama. Ni mabaya yalioje watakayo pewa!
 
100Hizi ni katika khabari za miji, tunakusimulia. Mingine ipo bado na mingine imefyekwa.
 
101Na Sisi hatukuwadhulumu, lakini wao wenyewe wamejidhulumu. Na miungu yao waliyo kuwa wakiiomba badala ya Mwenyezi Mungu haikuwafaa kitu ilipo kuja amri ya Mola wako Mlezi. Na hiyo miungu haikuwazidishia ila maangamizo tu.
 
102Na ndio kama hivyo ndivyo inavyo kuwa Mola wako Mlezi anapo ikamata miji inapo kuwa imedhulumu. Hakika mkamato wake ni mchungu na mkali.
 
103Hakika katika haya ipo ishara kwa yule anaye ogopa adhabu ya Akhera. Hiyo ndiyo Siku itakayo kusanyiwa watu, na hiyo ndiyo Siku itakayo shuhudiwa.
 
104Na Sisi hatuiakhirishi ila kwa muda unao hisabiwa.
 
105Siku hiyo itakapo fika, hatosema hata mtu mmoja ila kwa idhini yake Mwenyezi Mungu. Kati yao watakuwamo waliomo mashakani na wenye furaha.
 
106Ama wale wa mashakani hao watakuwamo Motoni wakiyayayatika na kukoroma.
 
107Watadumu humo muda wa kudumu mbingu na ardhi, isipo kuwa apendavyo Mola wako Mlezi. Hakika Mola wako Mlezi hutenda apendavyo.
 
108Na ama wale walio bahatika, wao watakuwamo Peponi wakidumu humo muda wa kudumu mbingu na ardhi, isipo kuwa apendavyo Mola wako Mlezi. Hicho ni kipawa kisio na ukomo.
 
109Basi usiwe na shaka juu ya wanayo yaabudu hao. Hawaabudu ila kama walivyo abudu baba zao zamani. Na hakika Sisi tutawatimilizia fungu lao bila ya kupunguzwa.
 
110Na kwa yakini tulimpa Musa Kitabu; zikazuka khitilafu ndani yake. Na lau kuwa si neno lilio kwisha tangulia kutoka kwa Mola wako Mlezi, bila ya shaka ingeli hukumiwa baina yao. Na hakika wao wamo katika shaka juu yake inayo wahangaisha.
 
111Na hakika Mola wako Mlezi atawatimilizia malipo ya vitendo vyao. Hakika Yeye anayo khabari ya wayatendayo.
 
112Basi, simama sawa sawa kama ulivyo amrishwa, wewe na wale wanao elekea kwa Mwenyezi Mungu pamoja nawe; wala msikiuke mipaka. Hakika Yeye anayaona yote myatendayo.
 
113Wala msiwategemee wanao dhulumu, usije ukakuguseni Moto. Wala nyinyi hamna walinzi badala ya Mwenyezi Mungu, wala tena hamtasaidiwa.
 
114Na shika Sala katika ncha mbili za mchana na nyakati za usiku zilizo karibu na mchana. Hakika mema huondoa maovu. Huu ni ukumbusho kwa wanao kumbuka.
 
115Na subiri, kwani Mwenyezi Mungu hapotezi ujira wa wanao fanya wema.
 
116Basi mbona hawakuwamo katika watu wa kabla yenu wenye vyeo na wasaa wanao kataza uharibifu katika nchi, isipo kuwa wachache tu, ambao ndio tulio waokoa? Na walio dhulumu walifuata starehe zao, na wakawa ni wakosefu.
 
117Wala hakuwa Mola wako Mlezi wa kuihiliki miji kwa dhulma tu na hali watu wake ni watenda mema.
 
118Na Mola wako Mlezi angeli penda ange wafanya watu wote wakawa umma mmoja. Lakini hawaachi kukhitalifiana,
 
119Isipo kuwa wale ambao Mola wako Mlezi amewarehemu; na kwa hiyo ndio Mwenyezi Mungu amewaumba. Na litatimia neno la Mola wako Mlezi: Kweli kweli nitaijaza Jahannam kwa majini na watu pamoja.
 
120Na yote tunayo kusimulia katika khabari za Mitume ni ya kukupa nguvu moyo wako. Na katika haya imekujia haki na mawaidha na ukumbusho kwa Waumini.
 
121Na waambie wale wasio amini: Fanyeni muwezavyo, nasi pia tunafanya.
 
122Na ngojeni, na sisi tunangoja.
 
123Na ni vya Mwenyezi Mungu tu vyote vilivyo fichikana katika ardhi na mbingu, na mambo yote yatarejezwa kwake. Basi muabudu Yeye na umtegemee Yeye. Na Mola wako Mlezi haghafiliki na yale mnayo yatenda.