63 - AL - MUNAAFIQUN |
|
|
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU. |
|
|
1 | Wanapo kujia wanaafiki husema: Tunashuhudia ya kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anajua kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu anashuhudia ya kuwa hakika wanaafiki ni waongo. |
|
2 | Wamevifanya viapo vyao ni kinga, na wao wakajizuia kuifuata Njia ya Mwenyezi Mungu. Hakika ni mabaya kabisa waliyo kuwa wakiyafanya. |
|
3 | Hayo ni kwa sababu ya kuwa waliamini, kisha wakakufuru; kwa hivyo umepigwa muhuri juu ya nyoyo zao. Kwa hivyo hawafahamu lolote. |
|
4 | Na unapo waona, miili yao inakupendeza, na wakisema, unasikiliza usemi wao. Lakini wao ni kama magogo yaliyo egemezwa. Wao hudhania kila ukelele unao pigwa ni kwa ajili yao. Hao ni maadui; tahadhari nao. Mwenyezi Mungu awaangamizilie mbali! Vipi wanapotoka na haki? |
|
5 | Na wanapo ambiwa: Njooni ili Mtume wa Mwenyezi Mungu akuombeeni maghfira, huvigeuza vichwa vyao, na unawaona wanageuka nao wamejaa kiburi. |
|
6 | Sawa sawa kwao, ukiwatakia maghfira au hukuwatakia maghfira, Mwenyezi Mungu hatawaghufiria. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wapotovu. |
|
7 | Hao ndio wanao sema: Msitoe mali kwa ajili ya walioko kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, ili waondokelee mbali! Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye khazina za mbingu na ardhi, lakini wanaafiki hawafahamu. |
|
8 | Wanasema: Tukirejea Madina mwenye utukufu zaidi bila ya shaka atamfukuza aliye mnyonge. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye utukufu - Yeye, na Mtume wake, na Waumini. Lakini wanaafiki hawajui. |
|
9 | Enyi mlio amini! Yasikusahaulisheni mali yenu, wala watoto wenu, kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Na wenye kufanya hayo ndio walio khasiri. |
|
10 | Na toeni katika tulicho kupeni kabla hayajamfikia mmoja wenu mauti, tena hapo akasema: Mola wangu Mlezi! Huniakhirishi muda kidogo nipate kutoa sadaka, na niwe katika watu wema? |
|
11 | Wala Mwenyezi Mungu hataiakhirisha nafsi yoyote inapo fika ajali yake; na Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda. |
|