54 - AL-QAMAR |
|
|
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU. |
|
|
1 | Saa imekaribia, na mwezi umepasuka! |
|
2 | Na wakiona Ishara hugeuka upande na husema: Huu uchawi tu unazidi kuendelea. |
|
3 | Na wamekanusha na wamefuata matamanio yao. Na kila jambo ni lenye kuthibiti. |
|
4 | Na bila ya shaka zimewajia khabari zenye makaripio. |
|
5 | Hikima kaamili; lakini maonyo hayafai kitu! |
|
6 | Basi jiepushe nao. Siku atakapo ita mwitaji kuliendea jambo linalo chusha; |
|
7 | Macho yao yatainama; watatoka makaburini kama nzige walio tawanyika, |
|
8 | Wanamkimbilia mwitaji, na makafiri wanasema: Hii ni siku ngumu. |
|
9 | Kabla yao kaumu ya Nuhu walikanusha; wakamkanusha mja wetu, na wakasema ni mwendawazimu, na akakaripiwa. |
|
10 | Basi akamwomba Mola wake Mlezi akasema: Kwa hakika mimi nimeshindwa, basi ninusuru! |
|
11 | Basi tukaifungua milango ya mbingu kwa maji yanayo miminika. |
|
12 | Na tukazipasua ardhi kwa chemchem, yakakutana maji kwa jambo lilio kadiriwa. |
|
13 | Na tukamchukua kwenye safina ya mbao na kamba. |
|
14 | Ikawa inakwenda kwa nadhari yetu, kuwa ni malipo kwa alivyo kuwa amekanushwa. |
|
15 | Na bila ya shaka tuliiacha iwe ni Ishara. Lakini je, yupo anaye kumbuka? |
|
16 | Basi ilikuwaje adhabu yangu, na maonyo yangu. |
|
17 | Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur'ani iwe nyepesi kufahamika. Lakini yupo anaye kumbuka? |
|
18 | Kina A'di walikanusha. Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu? |
|
19 | Hakika Sisi tuliwapelekea upepo wa kimbunga katika siku korofi mfululizo, |
|
20 | Ukiwang'oa watu kama vigogo vya mitende vilio ng'olewa. |
|
21 | Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu? |
|
22 | Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur'ani nyepesi kufahamika; lakini yupo anaye kumbuka? |
|
23 | Thamudi waliwakanusha Waonyaji. |
|
24 | Wakasema: Ati tumfuate binaadamu mmoja katika sisi? Basi hivyo sisi tutakuwa katika upotofu na kichaa! |
|
25 | Ni yeye tu aliye teremshiwa huo ukumbusho kati yetu sote? Bali huyu ni mwongo mwenye kiburi! |
|
26 | Kesho watajua ni nani huyo mwongo mwenye kiburi. |
|
27 | Hakika Sisi tutawapelekea ngamia jike ili kuwajaribu, basi watazame tu na ustahamili. |
|
28 | Na waambie kwamba maji yatagawanywa baina yao; kila sehemu ya maji itahudhuriwa na aliye khusika. |
|
29 | Basi wakamwita mtu wao akaja akamchinja. |
|
30 | Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu! |
|
31 | Hakika Sisi tuliwapelekea ukelele mmoja tu, wakawa kama mabuwa ya kujengea uwa. |
|
32 | Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur'ani iwe nyepesi kwa kukumbuka, lakini yupo akumbukaye? |
|
33 | Kaumu Lut'i nao waliwakadhibisha Waonyaji. |
|
34 | Hakika Sisi tukawapelekea kimbunga cha vijiwe, isipo kuwa wafuasi wa Lut'i. Hao tuliwaokoa karibu na alfajiri. |
|
35 | Kwa neema inayo toka kwetu. Hivyo ndivyo tumlipavyo anaye shukuru. |
|
36 | Na hakika yeye aliwaonya adhabu yetu; lakini wao waliyatilia shaka hayo maonyo. |
|
37 | Na walimtaka awape wageni wake. Tukayapofua macho yao, na tukawaambia: Onjeni basi adhabu na maonyo yangu! |
|
38 | Na iliwafikia wakati wa asubuhi adhabu yangu ya kuendelea. |
|
39 | Basi onjeni adhabu na maonyo yangu! |
|
40 | Na hakika tumeisahilisha Qur'ani kuikumbuka. Lakini yupo anaye kumbuka? |
|
41 | Na Waonyaji waliwafikia watu wa Firauni. |
|
42 | Walizikadhibisha Ishara zetu zote, nasi tukawashika kama anavyo shika Mwenye nguvu Mwenye uweza. |
|
43 | Je! Makafiri wenu ni bora kuliko hao, au yameandikwa vitabuni kuwa nyinyi hamtiwi makosani? |
|
44 | Au ndio wanasema: Sisi ni wengi tutashinda tu. |
|
45 | Wingi wao huu utashindwa, na wao watasukumwa nyuma. |
|
46 | Bali Saa ya Kiyama ndio miadi yao, na Saa hiyo ni nzito zaidi na chungu zaidi. |
|
47 | Hakika wakosefu wamo katika upotofu na wazimu. |
|
48 | Siku watakapo kokotwa Motoni kifudifudi waambiwe: Onjeni mguso wa Jahannamu! |
|
49 | Kwa hakika Sisi tumekiumba kila kitu kwa kipimo. |
|
50 | Na amri yetu haikuwa ila ni moja tu, kama kupepesa jicho. |
|
51 | Na bila ya shaka tumekwisha waangamiza wenzenu. Lakini yupo anaye kumbuka? |
|
52 | Na kila jambo walilo lifanya limo vitabuni. |
|
53 | Na kila kidogo na kikubwa kimeandikwa. |
|
54 | Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na mito. |
|
55 | Katika makalio ya haki kwa Mfalme Mwenye uweza. |
|