66 - ATTAH'RIIM |
|
|
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU. |
|
|
1 | Ewe Nabii! Kwa nini unaharimisha alicho kuhalilishia Mwenyezi Mungu? Unatafuta kuwaridhi wake zako. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. |
|
2 | Hakika Mwenyezi Mungu kakupeni Sharia ya kufungua viapo vyenu, na Mwenyezi Mungu ni Mola wenu. Na Yeye ni Mwenye kujua, Mwenye hikima. |
|
3 | Na Nabii alipo mwambia mmoja wa wake zake jambo la siri. Basi alipo litangaza yule mke, na Mwenyezi Mungu akamdhihirishia Mtume, alimjuvya sehemu na akaacha sehemu nyengine. Alipo mwambia hayo, huyo mke akasema: Nani aliye kwambia haya? Mtume akasema: Kaniambia Mjuzi Mwenye khabari zote! |
|
4 | Kama nyinyi wawili hamkutubia kwa Mwenyezi Mungu, basi nyoyo zenu zimekwisha elekea huko. Na mkisaidiana dhidi yake (Mtume), basi hakika Mwenyezi Mungu ndiye kipenzi chake, na Jibrili, na Waumini wema, na zaidi ya hayo Malaika pia watasaidia. |
|
5 | Asaa Mola wake Mlezi, akikupeni talaka, akampa wake wengine badala yenu nyinyi, walio bora kuliko nyinyi, wanynyekevu, Waumini, wat'awa, walio tubu, wenye kushika ibada, wafanyao kheri, wajane na wanawari. |
|
6 | Enyi mlio amini! Jilindeni nafsi zenu na ahali zenu na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe. Wanausimamia Malaika wakali, wenye nguvu, hawamuasi Mwenyezi Mungu kwa anayo waamrisha, na wanatenda wanayo amrishwa. |
|
7 | Enyi mlio kufuru! Msilete udhuru leo. Hakika mnalipwa mliyo kuwa mkiyatenda. |
|
8 | Enyi mlio amini! Tubuni kwa Mwenyezi Mungu toba iliyo ya kweli! Asaa Mola wenu Mlezi akakufutieni maovu yenu na akakuingizeni katika Pepo zipitazo mito kati yake, siku ambayo Mwenyezi Mungu hatamdhalilisha Nabii na walio amini pamoja naye. Nuru yao inakwenda mbele yao na pande zao za kulia, na huku wanasema: Mola wetu Mlezi! Tutimilizie nuru yetu, na utughufirie! Hakika Wewe ni Mwenye uweza juu ya kila kitu. |
|
9 | Ewe Nabii! Pambana na makafiri na wanaafiki, na kuwa mgumu kwao! Na makaazi yao ni Jahannamu. Na hayo ni marejeo mabaya. |
|
10 | Mwenyezi Mungu amewapigia mfano walio kufuru: mke wa Nuhu na mke wa Lut'i. Walikuwa chini ya waja wetu wema wawili miongoni mwa waja wetu. Lakini wakawakhuni waume zao, nao wasiwafae kitu. Na ikasemwa: Ingieni Motoni pamoja na wanao ingia! |
|
11 | Na Mwenyezi Mungu amewapigia mfano walio amini - mkewe Firauni, alipo sema: Mola wangu Mlezi! Nijengee kwako nyumba Peponi, na uniokoe na Firauni na vitendo vyake, na uniokoe na watu madhaalimu. |
|
12 | Na Mariamu binti wa Imrani, aliye linda ubikira wake, na tukampulizia humo kutoka roho yetu, na akayasadiki maneno ya Mola wake Mlezi na Vitabu vyake, na alikuwa miongoni mwa wat'iifu. |
|