37 - ASS'AFFAT |
|
|
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU. |
|
|
1 | Naapa kwa wanao jipanga kwa safu. |
|
2 | Na kwa wenye kukataza mabaya. |
|
3 | Na kwa wenye kusoma Ukumbusho. |
|
4 | Hakika Mungu wenu bila ya shaka ni Mmoja. |
|
5 | Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, na yaliyomo kati yao, na ni Mola Mlezi wa mashariki zote. |
|
6 | Hakika Sisi tumeipamba mbingu ya karibu kwa pambo la nyota. |
|
7 | Na kulinda na kila shet'ani a'si. |
|
8 | Wasiweze kuwasikiliza viumbe watukufu. Na wanafukuzwa huko kila upande. |
|
9 | Wakifurushwa. Na wanayo adhabu ya kudumu. |
|
10 | Isipo kuwa anaye nyakua kitu kidogo, na mara humfwatia kimondo kinacho ng'ara. |
|
11 | Hebu waulize: Je! Wao ni wenye umbo gumu zaidi au hao wengine tulio waumba. Hakika Sisi tuliwaumba wao kwa udongo unao nata. |
|
12 | Bali unastaajabu, na wao wanafanya maskhara. |
|
13 | Na wanapo kumbushwa hawakumbuki. |
|
14 | Na wanapo ona Ishara, wanafanya maskhara. |
|
15 | Na husema: Haya si chochote ila ni uchawi tu ulio dhaahiri. |
|
16 | Ati tukisha kufa na tukawa udongo na mifupa ndio kweli tutafufuliwa? |
|
17 | Hata baba zetu wa zamani? |
|
18 | Sema: Naam! Hali nanyi ni madhalili. |
|
19 | Huko utapigwa ukelele mmoja tu! Na hapo ndio wataona! |
|
20 | Watasema: Ole wetu! Hii ndiyo Siku ya Malipo. |
|
21 | Hii ndiyo Siku ya Hukumu mliyo kuwa mkiikadhibisha. |
|
22 | Wakusanyeni walio dhulumu, na wake zao, na hao walio kuwa wakiwaabudu - |
|
23 | Badala ya Mwenyezi Mungu. Waongozeni njia ya Jahannamu! |
|
24 | Na wasimamisheni. Hakika hao watasailiwa: |
|
25 | Mna nini? Mbona hamsaidiani? |
|
26 | Bali hii leo, watasalimu amri. |
|
27 | Watakabiliana wao kwa wao kuulizana. |
|
28 | Watasema: Kwa hakika nyinyi mlikuwa mkitujia upande wa kulia. |
|
29 | Watasema (wakubwa): Bali nyinyi wenyewe hamkuwa Waumini. |
|
30 | Sisi hatukuwa na mamlaka juu yenu, bali nyinyi wenyewe mlikuwa wapotovu. |
|
31 | Basi hukumu ya Mola wetu Mlezi imekwisha tuthibitikia. Hakika bila ya shaka tutaonja tu adhabu. |
|
32 | Tulikupotezeni kwa sababu sisi wenyewe tulikuwa wapotovu. |
|
33 | Basi wao kwa hakika siku hiyo watashirikiana katika adhabu pamoja. |
|
34 | Hivyo ndivyo tutakavyo wafanyia wakosefu. |
|
35 | Wao walipo kuwa wakiambiwa La ilaha illa 'Llahu Hapana mungu ila Mwenyezi Mungu tu, wakijivuna. |
|
36 | Na wakisema: Hivyo sisi tuiache miungu yetu kwa ajili ya huyu mtunga mashairi mwendawazimu? |
|
37 | Bali huyu amekuja kwa Haki, na amewasadikisha Mitume. |
|
38 | Hakika nyinyi bila ya shaka mtaionja adhabu chungu. |
|
39 | Wala hamlipwi ila hayo mliyo kuwa mkiyafanya. |
|
40 | Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio khitariwa. |
|
41 | Hao ndio watakao pata riziki maalumu, |
|
42 | Matunda, nao watahishimiwa. |
|
43 | Katika Bustani za neema. |
|
44 | Wako juu ya viti wamekabiliana. |
|
45 | Wanazungushiwa kikombe chenye kinywaji cha chemchem |
|
46 | Kinywaji cheupe, kitamu kwa wanywao. |
|
47 | Hakina madhara, wala hakiwaleweshi. |
|
48 | Na watakuwa nao wanawake wenye macho ya staha mazuri. |
|
49 | Hao wanawake kama mayai yaliyo hifadhika. |
|
50 | Waingie kuulizana wenyewe kwa wenyewe. |
|
51 | Aseme msemaji mmoja miongoni mwao: Hakika mimi nalikuwa na rafiki |
|
52 | Aliye kuwa akinambia: Hivyo wewe ni katika wanao sadiki |
|
53 | Ati tukisha kufa tukawa udongo na mafupa, ndio tutalipwa na kuhisabiwa? |
|
54 | Atasema: Je! Nyie mnawaona? |
|
55 | Basi atachungulia amwone katikati ya Jahannamu. |
|
56 | Atasema: Wallahi! Ulikaribia kunipoteza. |
|
57 | Na lau kuwa si neema ya Mola wangu Mlezi bila ya shaka ningeli kuwa miongoni mwa walio hudhurishwa. |
|
58 | Je! Sisi hatutakufa, |
|
59 | Isipo kuwa kifo chetu cha kwanza? Wala sisi hatutaadhibiwa. |
|
60 | Hakika huku bila ya shaka ndiko kufuzu kukubwa. |
|
61 | Kwa mfano wa haya nawatende watendao. |
|
62 | Je! Kukaribishwa hivi si ndio bora, au mti wa Zaqqum? |
|
63 | Hakika Sisi tumeufanya huo kuwa ni mateso kwa walio dhulumu. |
|
64 | Hakika huo ni mti unao toka katikati ya Jahannamu. |
|
65 | Mashada ya matunda yake kama kwamba vichwa vya mashet'ani. |
|
66 | Basi hakika bila ya shaka hao watayala hayo, na wajaze matumbo. |
|
67 | Kisha juu yake wanyweshwe mchanganyo wa maji yamoto yaliyo chemka. |
|
68 | Kisha hakika marejeo yao bila ya shaka yatakuwa kwenye Jahannamu. |
|
69 | Hakika waliwakuta baba zao wamepotea. |
|
70 | Na wao wakafanya haraka kufuata nyayo zao. |
|
71 | Na bila ya shaka walikwisha potea kabla yao wengi wa watu wa zamani. |
|
72 | Na Sisi hakika tuliwapelekea waonyaji. |
|
73 | Basi hebu angalia ulikuwaje mwisho wa walio onywa. |
|
74 | Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio khitariwa. |
|
75 | Na hakika Nuhu alitwita, na Sisi ni bora wa waitikiaji. |
|
76 | Na tulimwokoa yeye na ahali zake kutokana na msiba mkubwa. |
|
77 | Na tuliwajaalia dhuriya zake ndio wenye kubakia. |
|
78 | Na tukamwachia (sifa njema) kwa walio kuja baadaye. |
|
79 | Iwe salama kwa Nuhu ulimwenguni kote! |
|
80 | Kwa hakika hivi ndivyo tunavyo walipa wanao fanya mema. |
|
81 | Hakika yeye ni katika waja wetu walio amini. |
|
82 | Kisha tukawazamisha wale wengine. |
|
83 | Na hakika Ibrahim alikuwa katika kundi lake, |
|
84 | Alipo mjia Mola wake Mlezi kwa moyo mzima. |
|
85 | Alimwambia baba yake na watu wake: Mnaabudu nini? |
|
86 | Kwa kuzua tu mnataka miungu mingine badala ya Mwenyezi Mungu? |
|
87 | Mnamdhania nini Mola Mlezi wa walimwengu wote? |
|
88 | Kisha akapiga jicho kutazama nyota. |
|
89 | Akasema: Hakika mimi ni mgonjwa! |
|
90 | Nao wakamwacha, wakampa kisogo. |
|
91 | Basi akaiendea miungu yao kwa siri, akaiambia: Mbona hamli? |
|
92 | Mna nini hata hamsemi? |
|
93 | Kisha akaigeukia kuipiga kwa mkono wa kulia. |
|
94 | Basi wakamjia upesi upesi. |
|
95 | Akasema: Hivyo mnaviabudu vitu mnavyo vichonga wenyewe? |
|
96 | Na hali Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni nyinyi na hivyo mnavyo vifanya! |
|
97 | Wakasema: Mjengeeni jengo, na kisha mtupeni motoni humo! |
|
98 | Basi walitaka kumfanyia vitimbi, lakini tukawafanya wao ndio wa chini. |
|
99 | Na akasema: Hakika mimi nahama, nakwenda kwa Mola wangu Mlezi; Yeye ataniongoa. |
|
100 | Ewe Mola wangu Mlezi! Nitunukie aliye miongoni mwa watenda mema. |
|
101 | Basi tukambashiria mwana aliye mpole. |
|
102 | Basi alipo fika makamo ya kwenda na kurudi pamoja naye, alimwambia: Ewe mwanangu! Hakika mimi nimeona usingizini kuwa ninakuchinja. Basi angalia wewe, waonaje? Akasema: Ewe baba yangu! Tenda unavyo amrishwa, utanikuta mimi, Inshallah, katika wanao subiri. |
|
103 | Basi wote wawili walipo jisalimisha, na akamlaza juu ya kipaji. |
|
104 | Tulimwita: Ewe Ibrahim! |
|
105 | Umekwisha itimiliza ndoto. Hakika hivi ndivyo tunavyo walipa wanao tenda mema. |
|
106 | Hakika haya ni majaribio yaliyo dhaahiri. |
|
107 | Basi tukamtolea fidia kwa dhabihu mtukufu. |
|
108 | Na tukamwachia (sifa njema) kwa watu walio kuja baadaye. |
|
109 | Iwe salama kwa Ibrahim! |
|
110 | Hivi ndivyo tunavyo walipa wanao fanya mema. |
|
111 | Hakika yeye ni katika waja wetu walio amini. |
|
112 | Na tukambashiria kuzaliwa Is-haqa, naye ni Nabii miongoni mwa watu wema. |
|
113 | Na tukambarikia yeye na Is-haqa. Na miongoni mwa dhuriya zao walitokea wema na wenye kudhulumu nafsi zao waziwazi. |
|
114 | Na kwa hakika tuliwafanyia hisani Musa na Haruni. |
|
115 | Na tukawaokoa wao na watu wao kutokana na dhiki kubwa. |
|
116 | Na tukawanusuru; na wakawa wao ndio wenye kushinda. |
|
117 | Na tukawapa wawili hao Kitabu kinacho bainisha. |
|
118 | Na tukawaongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka. |
|
119 | Na tukawaachia (sifa njema) katika watu walio kuja baadaye. |
|
120 | Iwe salama kwa Musa na Haruni! |
|
121 | Hakika hivyo ndivyo tunavyo walipa walio wema. |
|
122 | Hakika wawili hao ni katika waja wetu walio amini. |
|
123 | Na hakika Ilyas bila ya shaka alikuwa miongoni mwa Mitume. |
|
124 | Alipo waambia watu wake: Hamwogopi? |
|
125 | Mnamwomba Baa'li na mnamwacha Mbora wa waumbaji, |
|
126 | Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wenu na Mola Mlezi wa baba zenu wa zamani? |
|
127 | Wakamkadhibisha. Basi kwa hakika watahudhurishwa; |
|
128 | Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio safishwa. |
|
129 | Na tumemwachia (sifa nzuri) kwa walio kuja baadaye. |
|
130 | Iwe salama kwa Ilyas. |
|
131 | Hakika hivyo ndivyo tunavyo walipa walio wema. |
|
132 | Hakika yeye ni katika waja wetu walio amini. |
|
133 | Na hakika Lut'i bila ya shaka ni miongoni mwa Mitume. |
|
134 | Tulipo mwokoa yeye na ahali zake wote, |
|
135 | Isipo kuwa mwanamke mkongwe katika wale walio bakia nyuma. |
|
136 | Kisha tukawaangamiza wale wengineo. |
|
137 | Na hakika nyinyi mnawapitia wakati wa asubuhi, |
|
138 | Na usiku. Basi je! Hamyatii akilini? |
|
139 | Na hakika Yunus alikuwa miongoni mwa Mitume. |
|
140 | Alipo kimbia katika jahazi lilio sheheni. |
|
141 | Akaingia katika kupigiwa kura, na akawa katika walio shindwa. |
|
142 | Samaki akammeza hali ya kuwa ni mwenye kulaumiwa. |
|
143 | Na ingeli kuwa hakuwa katika wanao mtakasa Mwenyezi Mungu, |
|
144 | Bila ya shaka angeli kaa ndani yake mpaka siku ya kufufuliwa. |
|
145 | Lakini tulimtupa ufukweni patupu, hali yu mgonjwa. |
|
146 | Na tukauotesha juu yake mmea wa kabila ya mung'unye. |
|
147 | Na tulimtuma kwa watu laki moja au zaidi. |
|
148 | Basi wakaamini, na tukawastarehesha kwa muda. |
|
149 | Basi waulize: Ati Mola wako Mlezi ndiye mwenye watoto wa kike, na wao wanao watoto wa kiume? |
|
150 | Au tumewaumba Malaika kuwa ni wanawake, na wao wakashuhudia? |
|
151 | Ati ni kwa uzushi wao ndio wanasema: |
|
152 | Mwenyezi Mungu amezaa! Ama hakika bila ya shaka hao ni waongo! |
|
153 | Ati amekhiari watoto wa kike kuliko wanaume? |
|
154 | Mna nini? Mnahukumu vipi nyinyi? |
|
155 | Hamkumbuki? |
|
156 | Au mnayo hoja iliyo wazi? |
|
157 | Basi leteni Kitabu chenu kama mnasema kweli. |
|
158 | Na wameweka makhusiano ya nasaba baina yake na majini; na majini wamekwisha jua bila ya shaka kuwa wao watahudhurishwa. |
|
159 | Subhana 'Llah Ametakasika Mwenyezi Mungu na hayo wanayo msingizia. |
|
160 | Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio safishwa. |
|
161 | Basi hakika nyinyi na mnao waabudu |
|
162 | Hamwezi kuwapoteza |
|
163 | Isipo kuwa yule atakaye ingia Motoni. |
|
164 | Na hapana katika sisi ila anapo mahali pake maalumu. |
|
165 | Na hakika bila ya shaka sisi ndio wajipangao safu. |
|
166 | Na hakika sisi ndio wenye kusabihi kutakasa. |
|
167 | Na walikuwapo walio kuwa wakisema: |
|
168 | Tungeli kuwa na Ukumbusho kama wa watu wa zamani, |
|
169 | Bila ya shaka tungeli kuwa ni waja wa Mwenyezi Mungu wenye ikhlasi. |
|
170 | Lakini waliukataa. Basi watakuja jua. |
|
171 | Na bila ya shaka neno letu lilikwisha tangulia kwa waja wetu walio tumwa. |
|
172 | Ya kuwa wao bila ya shaka ndio watakao nusuriwa. |
|
173 | Na kwamba jeshi letu ndilo litakalo shinda. |
|
174 | Basi waachilie mbali kwa muda. |
|
175 | Na watazame, nao wataona. |
|
176 | Je! Wanaihimiza adhabu yetu? |
|
177 | Basi itakapo shuka uwanjani kwao, itakuwa asubuhi mbaya kwa walio onywa. |
|
178 | Na waache kwa muda. |
|
179 | Na tazama, na wao wataona. |
|
180 | Subhana Rabbi'l'Izzat Ametakasika Mola Mlezi Mwenye enzi na yale wanayo mzulia. |
|
181 | Na Salamu juu ya Mitume. |
|
182 | Na sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote. |
|