52 - ATT'UR |
|
|
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU. |
|
|
1 | Naapa kwa mlima wa T'ur, |
|
2 | Na Kitabu kilicho andikwa |
|
3 | Katika ngozi iliyo kunjuliwa, |
|
4 | Na kwa Nyumba iliyo jengwa, |
|
5 | Na kwa dari iliyo nyanyuliwa, |
|
6 | Na kwa bahari iliyo jazwa, |
|
7 | Hakika adhabu ya Mola wako Mlezi hapana shaka itatokea. |
|
8 | Hapana wa kuizuia. |
|
9 | Siku zitakapo tikisika mbingu kwa mtikiso, |
|
10 | Na milima iwe inakwenda kwa mwendo mkubwa. |
|
11 | Basi ole wao siku hiyo hao wanao kadhibisha, |
|
12 | Ambao wanacheza katika mambo ya upuuzi. |
|
13 | Siku watapo sukumwa kwenye Moto kwa msukumo wa nguvu, |
|
14 | (Waambiwe): Huu ndio ule Moto mlio kuwa mkiukanusha! |
|
15 | Je! Huu ni uchawi, au hamwoni tu? |
|
16 | Uingieni, mkistahamili au msistahamili - ni mamoja kwenu. Hakika mnalipwa kwa mliyo kuwa mkiyatenda. |
|
17 | Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na neema, |
|
18 | Wakifurahi kwa yale aliyo wapa Mola wao Mlezi. Na Mola wao Mlezi atawalinda na adhabu ya Motoni. |
|
19 | Kuleni na kunyweni kwa raha kabisa kwa sababu ya mliyo kuwa mkiyatenda. |
|
20 | Watakuwa wameegemea juu ya viti vya enzi vilivyo pangwa kwa safu. Na tutawaoza mahuru-l-aini. |
|
21 | Na walio amini na dhuriya zao wakawafuata kwa Imani tutawakutanisha nao dhuriya zao, na wala hatutawapunja hata kidogo katika vitendo vyao. Kila mtu lazima atapata alicho kichuma. |
|
22 | Na tutawapa matunda, na nyama kama watavyo penda. |
|
23 | Watapeana humo bilauri zisio na vinywaji vya kuleta maneno ya upuuzi wala dhambi. |
|
24 | Iwe wanawapitia watumishi wao kama kwamba ni lulu zilizomo katika chaza. |
|
25 | Wataelekeana wakiulizana. |
|
26 | Waseme: Tulikuwa zamani pamoja na ahali zetu tukiogopa; |
|
27 | Basi Mwenyezi Mungu akatufanyia hisani na akatulinda na adhabu ya upepo wa Moto. |
|
28 | Hakika sisi zamani tulikuwa tukimwomba Yeye tu. Hakika Yeye ndiye Mwema Mwenye kurehemu. |
|
29 | Basi kumbusha! Kwani wewe, kwa neema ya Mola wako Mlezi, si kuhani wala mwendawazimu. |
|
30 | Au wanasema: Huyu ni mtunga mashairi, tunamtarajia kupatilizwa na dahari. |
|
31 | Sema: Tarajieni, na mimi pia ni pamoja nanyi katika kutarajia. |
|
32 | Au hizo akili zao ndio zinawaamrisha haya, au wao basi ni watu majeuri tu? |
|
33 | Au ndio wanasema: Ameitunga hii! Bali basi tu hawaamini! |
|
34 | Basi nawalete masimulizi kama haya ikiwa wao wanasema kweli. |
|
35 | Au wao wameumbwa pasipo kutokana na kitu chochote, au ni wao ndio waumbaji? |
|
36 | Au wao wameziumba mbingu na ardhi? Bali hawana na yakini. |
|
37 | Au wanazo khazina za Mola wako Mlezi au wao ndio wenye madaraka? |
|
38 | Au wanazo ngazi za kusikilizia? Basi huyo msikilizaji wao na alete hoja ilio wazi! |
|
39 | Au Yeye Mwenyezi Mungu ana wasichana, na nyinyi ndio mna wavulana? |
|
40 | Au wewe unawaomba ujira, na kwa hivyo ndio wanaelemewa na uzito wa gharama? |
|
41 | Au wanayo ilimu ya ghaibu, nao wameandika? |
|
42 | Au wanataka kufanya vitimbi tu? Lakini hao walio kufuru ndio watakao tegeka. |
|
43 | Au wanae mungu asiye kuwa Mwenyezi Mungu? Subhanallah! Ametaksika Mwenyezi Mungu na hao wanao washirikisha naye. |
|
44 | Na hata wange ona pande linatoka mbinguni linaanguka wange sema: Ni mawingu yaliyo bebana. |
|
45 | Basi waache mpaka wakutane na siku yao watakapo hilikishwa. |
|
46 | Siku ambayo hila zao hazitawafaa hata kidogo, wala wao hawatanusuriwa. |
|
47 | Na hakika walio dhulumu watapata adhabu nyengine isiyo kuwa hii, lakini wengi wao hawajui. |
|
48 | Na ingojee hukumu ya Mola wako Mlezi. Kwani wewe hakika uko mbele ya macho yetu, na mtakase kwa kumsifu Mola wako Mlezi unapo simama, |
|
49 | Na usiku pia mtakase, na zinapo kuchwa nyota. |
|