___Translations___

_Quran?_

_Gadgets_

_Search_

_Links_

_Contribute_

_Note_

1 - AL-FAATIH'A
2 - AL - BAQARA
3 - AL I'MRAN
4 - AN-NISAAI
5 - AL - MAIDA
6 - AL - AN-A'AM
7 - AL - A'RAAF
8 - AL - ANFAAL
9 - AT-TAWBA
10 - YUNUS
11 - HUD
12 - YUSUF
13 - AR-RAA'D
14 - IBRAHIM
15 - AL - HIJR
16 - AN NAH'L
17 - AL ISRAAI (BANI ISRAIL)
18 - AL - KAHF
19 - MARYAM
20 - T'AHA
21 - AL - ANBIYAA
22 - AL -HAJJ
23 - AL - MUUMINUN
24 - AN - NUR
25 - AL - FURQAN
26 - ASH-SHUA'RAA
27 - AN-NAML
28 - AL-QAS'AS'
29 - AL - A'NKABUT
30 - AR-RUM
31 - LUQMAN
32 - ASSAJDAH
33 - AL-AH'ZAB
34 - SABAA
35 - FAAT'IR
36 - YA-SIN
37 - ASS'AFFAT
38 - S'AAD
39 - AZZUMAR
40 - GHAAFIR (AU AL MUUMIN)
41 - FUSS'ILAT (AU H'A MIM SAJDAH)
42 - ASH-SHUURA
43 - AZZUKHRUF
44 - ADDUKHAN
45 - AL - JAATHIYA
46 - AL - AH'QAAF
47 - MUH'AMMAD
48 - AL FAT-H'I
49 - AL H'UJURAAT
50 - QAAF
51 - ADH-DHAARIYAAT
52 - ATT'UR
53 - ANNAJM
54 - AL-QAMAR
55 - ARRAH'MAN
56 - AL -WAAQIA'H
57 - AL -H'ADIID
58 - AL - MUJAADALAH
59 - AL - H'ASHRI
60 - AL - MUMTAH'INAH
61 - ASS'AF
62 - AL - JUMUA'
63 - AL - MUNAAFIQUN
64 - ATTAGHAABUN
65 - ATT'ALAAQ
66 - ATTAH'RIIM
67 - AL - MULK
68 - AL - QALAM
69 - AL - H'AAQQAH
70 - AL - MAA'RIJ
71 - NUH'
72 - AL - JINN
73 - AL - MUZZAMMIL
74 - AL - MUDDATHTHIR
75 - AL - QIYAMAH
76 - AL - INSAN
77 - AL - MURSALAAT
78 - ANNABAA
79 - ANNAZIA'AT
80 - A'BASA
81 - ATTAKWIR
82 - AL - INFIT'AAR
83 - AL - MUT'AFFIFIIN
84 - AL - INSHIQAAQ
85 - AL - BURUUJ
86 - ATT'AARIQ
87 - AL - AA'LAA
88 - AL - GHAASHIYAH
89 - AL - FAJR
90 - AL - BALAD
91 - ASH-SHAMS
92 - AL - LAYL
93 - WADH-DHUH'AA
94 - ASH-SHARH'
95 - AT-TIN
96 - AL - A'LAQ
97 - AL - QADR
98 - AL - BAYYINAH
99 - AZ-ZILZALAH
100 - AL - A'ADIYAAT
101 - AL - QAARIA'H
102 - AT-TAKAATHUR
103 - AL - A'S'R
104 - AL - HUMAZAH
105 - AL - FIIL
106 - QURAISH
107 - AL - MAAU'N
108 - AL - KAWTHAR
109 - AL - KAFIRUN
110 - ANNAS'R
111 - AL - MASAD
112 - AL - IKHLAS'
113 - AL - FALAQ
114 - ANNAS
KISWAHILI

12 - YUSUF

 

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.

 
1Alif Lam Raa. Hizi ni Aya za Kitabu kinacho bainisha.
 
2Hakika Sisi tumeiteremsha Qur'ani kwa Kiarabu ili mpate kuzingatia.
 
3Sisi tunasimulia simulizi nzuri kwa kukufunulia Qur'ani hii. Na ijapo kuwa kabla ya haya ulikuwa miongoni mwa wasio jua.
 
4Yusuf alipo mwambia baba yake: Ewe babaangu! Hakika mimi nimeota nyota kumi na moja, na jua, na mwezi. Nimeota zikinisujudia.
 
5(Baba) akasema: Ewe mwanangu! Usiwasimulie nduguzo ndoto yako, wasije wakakufanyia vitimbi. Hakika Shet'ani ni adui aliye dhaahiri kwa mwanaadamu.
 
6Na kadhaalika Mola wako Mlezi atakuteuwa na atakufundisha tafsiri ya mambo. Na atatimiza neema zake juu yako na juu ya ukoo wa Yaa'qub, kama alivyo watimizia hapo zamani baba zako Ibrahim na Is-haq. Hakika Mola wako Mlezi ni Mjuzi Mwenye hikima.
 
7Kwa yakini katika Yusuf na nduguze ziko ishara kwa wanao uliza.
 
8Pale walipo sema: Hakika Yusuf na nduguye wanapendwa zaidi na baba yetu kuliko sisi, hali sisi ni kikundi chenye nguvu. Hakika baba yetu yumo katika upotofu wa dhaahiri.
 
9Muuweni Yusuf, au mtupeni nchi mbali ili uso wa baba yenu ukuelekeeni nyinyi. Na baada ya haya mtakuwa watu wema.
 
10Akasema msemaji kati yao: Msimuuwe Yusuf. Lakini mtumbukizeni ndani ya kisima. Wasafiri watakuja mwokota; kama nyinyi mna sharti ya kufanya jambo.
 
11Wakasema: Ewe baba yetu! Una nini hata hutuamini kwa Yusuf? Na hakika sisi ni wenye kumtakia kheri!
 
12Mpeleke kesho pamoja nasi, ale kwa furaha na acheze; na bila ya shaka sisi tutamhifadhi.
 
13Akasem: Kwa hakika inanihuzunisha kwamba nyinyi mwende naye, na ninaogopa asije mbwa mwitu akamla nanyi mmeghafilika naye.
 
14Wakasema: Ikiwa mbwa mwitu atamla na hali sisi ni kundi lenye nguvu kabisa, basi bila ya shaka sisi tutakuwa khasarani.
 
15Basi walipo mchukua na wakakubaliana wamtumbukize ndani ya kisima, tulimfunulia Yusuf: Hapana shaka yoyote utakuja waambia kwa jambo lao hili, na wala wao hawatambui.
 
16Wakaja kwa baba yao usiku wakilia.
 
17Wakasema: Ewe baba yetu! Hakika tulikwenda kushindana na tukamwacha Yusuf penye vitu vyetu. Basi mbwa mwitu akamla. Lakini wewe hutuamini ijapo kuwa tunasema kweli.
 
18Wakaja na kanzu yake ina damu ya uwongo. Akasema: Bali nafsi zenu zimekushawishini kutenda kitendo. Lakini subira ni njema; na Mwenyezi Mungu ndiye wa kuombwa msaada kwa haya mnayo yaeleza.
 
19Ukafika msafara, wakamtuma mchota maji wao, naye akatumbukiza ndoo yake. Alisema: Kheri Inshallah! Huyu hapa mvulana! Wakamficha ili kumfanya ni bidhaa. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa wanayo yatenda.
 
20Na wakamuuza kwa thamani duni, kwa akali ya pesa. Wala hawakuwa na haja naye.
 
21Na yule aliye mnunua huko Misri alimwambia mkewe: Mtengenezee makaazi ya hishima huyu; huenda akatufaa au tukamfanya mwenetu. Na kama hivyo tulimweka Yusuf katika nchi ili tumfundishe kufasiri mambo. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kushinda katika jambo lake, lakini watu wengi hawajui.
 
22Na alipo fikilia utu uzima tulimpa hukumu na ilimu. Na kama hivi tunawalipa wanao tenda mema.
 
23Na yule bibi wa nyumba aliyo kuwamo Yusuf alimtamani kinyume cha nafsi yake, na akafunga milango. Akamwambia: Njoo! Yusuf akasema: Audhubillahi! Najikinga na Mwenyezi Mungu. Huyu bwana wangu kaniweka maskani nzuri, na hakika wenye kudhulumu hawatengenekewi.
 
24Na hakika yule mwanamke alimtamani, na Yusuf angeli mtamani lau kuwa hakuona ishara ya Mola wake Mlezi. Hayo hivyo ni kwa ajili tumuepushe na uovu na uchafu. Hakika yeye alikuwa katika waja wetu walio safishwa.
 
25Na wote wawili wakakimbilia mlangoni, na mwanamke akairarua kanzu yake Yusuf kwa nyuma. Na wakamkuta bwana wake mlangoni. Mwanamke akasema: Hapana malipo ya mwenye kutaka kumfanyia maovu mkeo isipo kuwa kufungwa au kupewa adhabu chungu.
 
26Yusuf akasema: Yeye ndiye aliye nitaka bila ya mimi kumtaka. Na shahidi aliye kuwa katika jamaa za mwanamke alisema: Ikiwa kanzu yake imechanwa mbele basi mwanamke amesema kweli, naye Yusuf ni katika waongo.
 
27Na ikiwa kanzu yake imechanwa nyuma, basi mwanamke amesema uwongo, naye Yusuf ni katika wakweli.
 
28Basi yule bwana alipoona kanzu yake imechanwa kwa nyuma, alisema: Hakika haya ni katika vitimbi vyenu wanawake. Bila ya shaka vitimbi vyenu ni vikuu.
 
29Yusuf! Wachilia mbali haya. Na wewe, mwanamke, omba msamaha kwa dhambi zako. Kwa hakika wewe ni katika walio fanya makosa.
 
30Na wanawake wa mjini wakawa wanasema: Mke wa Mheshimiwa anamtamani mtumishi wake ! Hakika amesalitika kwa mapenzi. Sisi hakika tunamwona yumo katika upotovu ulio dhaahiri.
 
31Alipo sikia yule bibi masengenyo yao aliwaita, na akawawekea matakia ya kuegemea, na akampa kila mmoja wao kisu. Akamwambia Yusuf: Tokeza mbele yao. Basi walipo mwona waliona ni kitu kikubwa kabisa, na wakajikata mikono yao. Wakasema: Hasha Lillahi! Huyu si mwanaadamu. Hakuwa huyu ila ni Malaika mtukufu.
 
32Yule bibi aksema: Huyu basi ndiye huyo mliye nilaumia! Na kweli mimi nilimtaka naye akakataa. Na akitofanya ninayo muamrisha basi hapana shaka atafungwa gerezani, na atakuwa miongoni mwa walio chini kabisa.
 
33Yusuf akasema: Ee Mola Mlezi wangu! Nastahabu kifungo kuliko haya anayo niitia. Na usipo niondoshea vitimbi vya wanawake mimi nitamili kwao, na nitakuwa katika wajinga.
 
34Basi Mola wake Mlezi akamwitikia, na akamwondoshea vitimbi vyao. Hakika Yeye ni Msikizi Mjuzi.
 
35Basi ikawadhihirikia baada ya kuona Ishara kuwa wamfunge kwa muda.
 
36Wakaingia gerezani pamoja naye vijana wawili. Mmoja wao akasema: Hakika mimi nimeota nakamua mvinyo. Na mwingine akasema: Mimi nimeota nimebeba mikate juu ya kichwa changu, na ndege wanaila. Hebu tuambie tafsiri yake, kwani sisi tunakuona wewe ni katika watu wema.
 
37Akasema: Hakitakufikilieni chakula mtakacho pewa ila nitakwambieni hakika yake kabla hakijakufikieni. Haya ni katika yale aliyo nifundisha Mola wangu Mlezi. Hakika mimi nimeacha mila ya watu wasio muamini Mwenyezi Mungu, na wakawa hawaiamini Akhera.
 
38Na nimefuata mila ya baba zangu, Ibrahim, na Is-haq, na Yaa'qub. Hatuna haki ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu na chochote. Hiyo ni katika fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yetu na juu ya watu; lakini watu wengi hawashukuru.
 
39Enyi wafungwa wenzangu wawili! Je, mabwana wengi wanao farikiana wao kwa wao ni bora au Mwenyezi Mungu Mmoja Mwenye nguvu?
 
40Hamuabudu badala yake ila majina tu mliyo yapanga nyinyi na baba zenu. Mwenyezi Mungu hakuyateremshia hayo uthibitisho wowote. Hapana hukumu ila ya Mwenyezi Mungu tu. Yeye ameamrisha msimuabudu yeyote isipo kuwa Yeye tu. Hiyo ndiyo Dini Iliyo Nyooka. Lakini watu wengi hawajui.
 
41Enyi wafungwa wenzangu wawili! Ama mmoja wenu atamnywesha bwana wake mvinyo. Na ama mwengine atasulubiwa, na ndege watamla kichwa chake. Imekwisha katwa hukumu ya hilo jambo mlilo kuwa mkiuliza.
 
42Na akamwambia yule aliye jua kuwa atavuka katika wale wawili: Nikumbuke kwa bwana wako. Lakini Shet'ani alimsahaulisha kumtaja kwa bwana wake. Basi Yusuf akakaa gerezani miaka kadhaa.
 
43Na siku moja mfalme alisema: Hakika mimi nimeota ng'ombe saba wanene wanaliwa na ng'ombe saba walio konda. Na mashuke saba mabichi na mengine makavu. Enyi waheshimiwa! Nambieni maana ya ndoto zangu, ikiwa nyinyi mnaweza kuagua ndoto.
 
44Wakasema: Hizi ni ndoto zilizo paraganyika, wala sisi sio wenye kujua tafsiri ya ndoto hizi.
 
45Hapo akasema yule aliye okoka katika wale wawili akakumbuka baada ya muda: Mimi nitakwambieni tafsiri yake. Basi nitumeni.
 
46Yusuf! Ewe mkweli! Tueleze nini maana ya ng'ombe saba wanene kuliwa na ng'ombe saba walio konda. Na mashuke saba mabichi na mengine makavu, ili nirejee kwa watu wapate kujua.
 
47Akasema: Mtalima miaka saba kwa juhudi. Mtacho vuna kiwacheni katika mashuke yake, isipo kuwa kidogo mtacho kula.
 
48Kisha itakuja baadaye miaka saba ya shida itakayo kula kile mlicho iwekea isipo kuwa kidogo mtacho kihifadhi.
 
49Kisha baada ya haya utakuja mwaka ambao katika mwaka huo watu watasaidiwa, na watakamua.
 
50Na mfalme akasema: Mleteni kwangu! Basi mjumbe alipo mjia Yusuf alisema: Rejea kwa bwana wako ukamuulize khabari ya wale wanawake walio jikata mikono yao. Hakika Mola wangu Mlezi anazijua vyema hila zao.
 
51Mfalme alisema: Mlikuwa mna nini mlipo mtaka Yusuf kinyume na nafsi yake? Wakasema: Hasha Lillahi! Sisi hatukujua ubaya wowote kwake. Mke wa Mheshimiwa akasema: Sasa haki imedhihiri. Mimi ndiye niliye mtaka kinyume na nafsi yake, na hakika yeye ni katika wakweli.
 
52Hayo ni apate kujua ya kwamba mimi sikumfanyia khiyana nyuma yake; na ya kwamba Mwenyezi Mungu haziongoi hila za makhaini.
 
53NAMI sijitoi lawamani. Kwa hakika nafsi ni mno kuamrisha maovu, isipo kuwa ile ambayo Mola wangu Mlezi aliyo irehemu. Hakika Mola wangu Mlezi ni Msamehevu na Mwenye kurehemu.
 
54Basi mfalme akasema: Mleteni kwangu, awe wangu mwenyewe khasa. Basi alipo msemeza alinena: Hakika wewe leo umekwisha tamakani kwetu na umeaminika.
 
55Yusuf akasema: Nifanye mshika khazina za nchi. Kwani hakika mimi ni mlinzi mjuzi.
 
56Basi namna hivi tukampa Yusuf cheo katika nchi; anakaa humo popote anapo penda. Tunamfikishia rehema zetu tumtakaye, wala hatupuuzi malipo ya wafanyao mema.
 
57Na hakika malipo ya Akhera ni bora zaidi, kwa walio amini na wakawa wachamngu.
 
58Wakaja ndugu zake Yusuf, na wakaingia kwake. Yeye akawajua na wao hawakumjua.
 
59Na alipo watengenezea tayari haja yao alisema: Nileteeni ndugu yenu kwa baba. Je! Hamwoni ya kwamba mimi ninatimiza kipimo, nami ni mbora wa kukirimu?
 
60Na msipo niletea basi hampati kipimo chochote kwangu, wala msinikurubie.
 
61Wakasema: Sisi tutamrairai baba yake; na bila ya shaka tutafanya hayo.
 
62Na Yusuf akawaambia watumishi wake: Tieni bidhaa zao katika mizigo yao, ili wazione watakapo rudi kwa watu wao wapate kurejea tena.
 
63Basi walipo rejea kwa baba yao, walisema: Ewe baba yetu! Tumenyimwa chakula zaidi, basi mpeleke nasi ndugu yetu ili tupate kupimiwa; na yakini sisi tutamlinda.
 
64Je, nikuaminini kwa huyu ila kama nilivyo kuaminini kwa nduguye zamani? Lakini Mwenyezi Mungu ndiye Mbora wa kulinda, naye ndiye Mbora wa kurehemu kuliko wenye kurehemu wote.
 
65Na walipo fungua mizigo yao wakakuta bidhaa zao wamerudishiwa. Wakasema: Ewe baba yetu! Tutake nini zaidi? Hizi bidhaa zetu tumerudishiwa. Wacha tuwaletee watu wetu chakula, na tutamlinda ndugu yetu, na tutaongeza shehena ya ngamia. Na hicho ni kipimo kidogo.
 
66Akasema: Sitampeleka nanyi mpaka mnipe ahadi kwa Mwenyezi Mungu kwamba lazima mtamrejeza kwangu, ila ikiwa mmezungukwa. Basi walipo mpa ahadi yao alisema: Mwenyezi Mungu ndiye Mtegemewa kwa tuyasemayo.
 
67Na akasema: Enyi wanangu! Msiingie mlango mmoja, bali ingieni kwa milango mbali mbali. Wala mimi sikufaeni kitu mbele ya Mwenyezi Mungu. Hukumu haiko ila kwa Mwenyezi Mungu tu. Juu yake Yeye mimi nimetegemea, na juu yake Yeye wategemee wanao tegemea.
 
68Na walipo ingia kama alivyo waamrisha baba yao, haikuwafaa kitu kwa Mwenyezi Mungu, isipo kuwa ni haja tu iliyo kuwa katika nafsi ya Yaa'qub aliitimiza. Na hakika yeye alikuwa na ilimu kwa sababu tulimfundisha; lakini watu wengi hawajui.
 
69Na walipo ingia kwa Yusuf alimchukua nduguye akasema: Mimi hakika ni nduguyo. Basi usihuzunike kwa waliyo kuwa wakiyafanya .
 
70Na alipo kwisha watengenezea mahitaji yao akakitia kikopo cha kunywea maji katika mzigo wa nduguye huyo, kisha mnadi akanadi: Enyi wasafiri! Hapana shaka nyinyi ni wezi!
 
71Wakasema nao wamewakabili: Kwani mmepoteza nini?
 
72Wakasema: Tumepoteza kopo la mfalme. Na ataye lileta atapewa shehena nzima ya ngamia. Nami ni dhaamini wa hayo.
 
73Wakasema: Wallahi! Mnajua vyema kwamba sisi hatukuja kufanya uharibifu katika nchi hii, wala sisi si wezi.
 
74Wakasema: Basi malipo yake yatakuwa nini ikiwa nyinyi ni waongo?
 
75Wakasema: Malipo yake ni yule ambaye ataonekana nalo yeye huyo ndiye malipo yake. Hivi ndivyo tunavyo walipa madhaalimu.
 
76Basi akaanza kwenye mizigo yao kabla ya mzigo wa nduguye. Kisha akakitoa katika mzigo wa nduguye. Hivi ndivyo tulivyo mpangia Yusuf. Hakuweza kumzuia nduguye kwa sharia ya mfalme isipo kuwa alivyo taka Mwenyezi Mungu. Tunawatukuza kwenye vyeo tuwatakao; na juu ya kila ajuaye yupo ajuaye zaidi.
 
77Wakasema: Ikiwa huyu ameiba, basi nduguye vile vile aliiba zamani. Lakini Yusuf aliyaweka siri moyoni mwake wala hakuwaonyesha. Akawaambia: Nyinyi mko katika hali mbaya zaidi, na Mwenyezi Mungu anajua zaidi hayo mnayo singizia.
 
78Wakasema: Ewe Mheshimiwa! Huyu anaye baba mzee sana. Kwa hivyo mchukue mmoja wetu badala yake. Hakika sisi tunakuona wewe ni katika watu wema.
 
79Akasema: Mwenyezi Mungu apishe mbali kumshika yeyote yule isipo kuwa tuliye mkuta naye kitu chetu. Hivyo basi tutakuwa wenye kudhulumu.
 
80Walipo kata tamaa naye wakenda kando kunong'ona. Mkubwa wao akasema: Je! Hamjui ya kwamba baba yenu amechukua ahadi kwenu kutokana na Mwenyezi Mungu, na kabla ya hapo mlimkosa katika agano lenu juu ya Yusuf? Basi mimi sitotoka nchi hii mpaka baba yangu anipe ruhusa au Mwenyezi Mungu anihukumie. Na Yeye ndiye Mbora wa mahakimu.
 
81Rudini kwa baba yenu, na mwambieni: Ee baba yetu! Mwanao ameiba. Na sisi hatutoi ushahidi ila kwa tunayo yajua. Wala sisi hatukuwa wenye kuhifadhi mambo ya ghaibu.
 
82Na waulize watu wa mji tulio kuwako, na msafara tulio kuja nao. Na hakika sisi tunasema kweli.
 
83Akasema: Bali nafsi zenu zimekushawishini kwenye jambo fulani. Subira ni njema! Asaa Mwenyezi Mungu akaniletea wote pamoja. Hakika Yeye ni Mjuzi Mwenye hikima.
 
84Naye akajitenga nao, na akasema: Ah! Masikini Yusuf! Na macho yake yakawa meupe kwa huzuni aliyo kuwa akiizuia.
 
85Wakasema: Wallahi! Huachi kumkumbuka Yusuf mpaka uwe mgonjwa au uwe katika walio hiliki.
 
86Akasema: Hakika mimi namshitakia Mwenyezi Mungu sikitiko langu na huzuni yangu. Na ninajua kwa Mwenyezi Mungu msiyo yajua nyinyi.
 
87Enyi wanangu! Nendeni mkamtafute Yusuf na nduguye, wala msikate tamaa na faraji ya Mwenyezi Mungu. Hakika hawakati tamaa na faraji ya Mwenyezi Mungu isipo kuwa watu makafiri.
 
88Basi walipo ingia kwa Yusuf walisema: Ewe Mheshimiwa! Imetupata shida, sisi na watu wetu. Na tumeleta mali kidogo. Basi tupimie kipimo na fanya kama unatupa sadaka. Hakika Mwenyezi Mungu huwalipa watoao sadaka.
 
89Akasema: Je! Mmejua mliyo mfanyia Yusuf na nduguye mlipo kuwa wajinga?
 
90Wakasema: Kumbe wewe ndiye Yusuf? Akasema: Mimi ndiye Yusuf, na huyu ni ndugu yangu. Mwenyezi Mungu ametufanyia hisani. Hakika anaye mcha Mungu na akasubiri, basi Mwenyezi Mungu haachi ukapotea ujira wa wafanyao mema.
 
91Wakasema: Wallahi! Mwenyezi Mungu amekufadhilisha wewe kuliko sisi, na hakika sisi tulikuwa wenye kukosa.
 
92Akasema: Leo hapana lawama juu yenu. Mwenyezi Mungu atakusameheni, naye ni Mwingi wa kurehemu kuliko wote wanao rehemu.
 
93Nendeni na kanzu yangu hii na mumwekee usoni baba yangu, atakuwa mwenye kuona. Na mje nao watu wenu wote wa nyumbani.
 
94Na ulipo ondoka tu msafara baba yao alisema: Hakika mimi nasikia harufu ya Yusuf, lau kuwa hamtanituhumu.
 
95Wakasema: Wallahi! Hakika bado ungali katika upotovu wako wa zamani.
 
96Basi alipo fika mbashiri na akaiweka kanzu usoni pake alirejea kuona. Akasema: Je! Sikukwambieni kuwa mimi najua ya Mwenyezi Mungu msiyo yajua nyinyi?
 
97Wakasema: Ee baba yetu! Tuombee msamaha kwa dhambi zetu. Hapana shaka sisi tulikuwa na makosa.
 
98Akasema: Nitakuja kuombeeni msamaha kwa Mola wangu Mlezi. Hakika Yeye ndiye Mwenye maghfira na Mwenye kusamehe.
 
99Na walipo ingia kwa Yusuf aliwakumbatia wazazi wake na akasema: Ingieni Misri, Inshallah, mmo katika amani.
 
100Na akawapandisha wazazi wake kwenye kiti cha enzi. Na wote wakaporomoka kumsujudia. Na akasema: Ewe baba yangu! Hii ndiyo tafsiri ya ile ndoto yangu ya zamani. Na Mwenyezi Mungu ameijaalia iwe kweli. Na Mwenyezi Mungu amenifanyia wema kunitoa gerezani, na kukuleteni kutoka jangwani baada ya Shet'ani kuchochea baina yangu na ndugu zangu. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mpole kwa alitakalo. Bila ya shaka Yeye ni Mjuzi Mwenye hikima.
 
101Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika umenipa utawala, na umenifunza tafsiri ya mambo. Ewe Muumba wa mbingu na ardhi! Wewe ndiye Mlinzi wangu katika dunia na Akhera. Nifishe hali ya kuwa ni Muislamu na nichanganyishe na watendao mema.
 
102Hizi ni katika khabari za ghaibu tulizo kufunulia. Na hukuwa pamoja nao walipo azimia shauri yao, walipo fanya njama zao wakizua vitimbi.
 
103Na wengi wa watu si wenye kuamini hata ukijitahidi vipi..
 
104Wala wewe huwaombi ujira kwa haya. Hayakuwa haya ila ni mawaidha kwa walimwengu wote.
 
105Na ishara ngapi katika mbingu na ardhi wanazo zipitia, na hali ya kuwa wanazipuuza.
 
106Na wengi katika wao hawamuamini Mwenyezi Mungu pasina kuwa ni washirikina.
 
107Je! Wanaaminisha kuwa haitowajia adhabu ya Mwenyezi Mungu ya kuwagubika, au haitawafikia Saa ya Kiyama kwa ghafla, na hali hawatambui?
 
108Sema: Hii ndiyo Njia yangu - ninalingania kwa Mwenyezi Mungu kwa kujua - mimi na wanao nifuata. Na ametakasika Mwenyezi Mungu! Wala mimi si katika washirikina.
 
109Na hatukuwatuma Mitume kabla yako isipo kuwa wanaume tulio wafunulia wahyi miongoni mwa watu wa mijini. Je! Hawatembei katika ardhi wakaona jinsi ulivyo kuwa mwisho wa walio kuwa kabla yao? Na hakika nyumba ya Akhera ni bora kwa wamchao Mungu. Basi hamfahamu?
 
110Hata Mitume walipo kata tamaa na wakaona kuwa wamekadhibishwa, hapo ikawajia nusura yetu, wakaokolewa tuwatakao. Na adhabu yetu haitowawacha kaumu ya wakosefu.
 
111Kwa hakika katika hadithi zao limo zingatio kwa wenye akili. Si maneno yaliyo zuliwa, bali ni ya kusadikisha yaliyo kabla yake, na ufafanuzi wa kila kitu, na ni uwongofu na rehema kwa kaumu yenye kuamini.