76 - AL - INSAN |
|
|
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU. |
|
|
1 | Hakika kilimpitia binaadamu kipindi katika zama ambacho kwamba hakuwa kitu kinacho tajwa. |
|
2 | Hakika Sisi tumemuumba mtu kutokana na mbegu ya uhai iliyo changanyika, tumfanyie mtihani. Kwa hivyo tukamfanya mwenye kusikia, mwenye kuona. |
|
3 | Hakika Sisi tumembainishia Njia. Ama ni mwenye kushukuru, au mwenye kukufuru. |
|
4 | Hakika Sisi tumewaandalia makafiri minyororo na pingu na Moto mkali. |
|
5 | Hakika watu wema watakunywa katika vinywaji vilivyo changanyika na kafuri, |
|
6 | Ni chemchem watakao inywa waja wa Mwenyezi Mungu, wakiifanya imiminike kwa wingi. |
|
7 | Wanatimiza ahadi, na wanaiogopa siku ambayo shari yake inaenea sana, |
|
8 | Na huwalisha chakula, juu ya kukipenda kwake, masikini, na yatima, na wafungwa. |
|
9 | Hakika sisi tunakulisheni kwa wajihi wa Mwenyezi Mungu. Hatutaki kwenu malipo wala shukrani. |
|
10 | Hakika sisi tunaiogopa kwa Mola wetu Mlezi hiyo siku yenye shida na taabu. |
|
11 | Basi Mwenyezi Mungu atawalinda na shari ya siku hiyo, na atawakutanisha na raha na furaha. |
|
12 | Na atawajazi Bustani za Peponi na maguo ya hariri kwa vile walivyo subiri. |
|
13 | Humo wataegemea juu ya viti vya enzi, hawataona humo jua kali wala baridi kali. |
|
14 | Na vivuli vyake vitakuwa karibu yao, na mashada ya matunda yataning'inia mpaka chini. |
|
15 | Na watapitishiwa vyombo vya fedha na vikombe vya vigae, |
|
16 | Vya fedha safi kama kiyoo, wamevipima kwa vipimo. |
|
17 | Na humo watanyweshwa kinywaji kilicho changanyika na tangawizi. |
|
18 | Hiyo ni chemchem iliyo humo inaitwa Salsabil. |
|
19 | Na watawazungukia kuwatumikia wavulana wasio pevuka, ukiwaona utawafikiri ni lulu zilizo tawanywa. |
|
20 | Na utakapo yaona, utakuwa umeona neema na ufalme mkubwa. |
|
21 | Juu yao zipo nguo za hariri laini za kijani kibichi, na hariri nzito ya at'ilasi. Na watavikwa vikuku vya fedha, na Mola wao Mlezi atawanywesha kinywaji safi kabisa. |
|
22 | Hakika haya ni malipo yenu; na juhudi zenu zimekubaliwa. |
|
23 | Hakika Sisi tumekuteremshia Qur'ani kidogo kidogo. |
|
24 | Basi ngojea hukumu ya Mola wako Mlezi wala usimt'ii miongoni mwao mwenye dhambi au mwenye kufuru. |
|
25 | Na likumbuke jina la Mola wako Mlezi asubuhi na jioni; |
|
26 | Na usiku msujudie Yeye, na umtakase usiku, wakati mrefu. |
|
27 | Kwa hakika watu hawa wanapenda maisha ya kidunia, na wanaiacha nyuma yao siku nzito. |
|
28 | Sisi tumewaumba, na tukavitia nguvu viungo vyao. Na tukitaka tutawabadilisha mfano wao wawe badala yao. |
|
29 | Hakika haya ni mawaidha; basi anaye taka atashika Njia ya kwenda kwa Mola wake Mlezi. |
|
30 | Wala hamwezi kutaka ila atakapo Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye ilimu, Mwenye hikima. |
|
31 | Humuingiza amtakaye katika rehema yake. Na wenye kudhulumu amewawekea adhabu iliyo chungu. |
|