43 - AZZUKHRUF |
|
|
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU. |
|
|
1 | H'a Mim |
|
2 | Naapa kwa Kitabu kinacho bainisha. |
|
3 | Hakika Sisi tumeifanya Qur'ani kwa Kiarabu ili mfahamu. |
|
4 | Na hakika hiyo imo katika Asili ya Maandiko yalioko kwetu, ni tukufu na yenye hikima. |
|
5 | Je! Tuache kukukumbusheni kabisa kwa kuwa nyinyi ni watu mlio pita mipaka kwa ukafiri? |
|
6 | Na Manabii wangapi tuliwatuma kwa watu wa zamani! |
|
7 | Na hawajii Nabii yeyote ila walikuwa wakimkejeli. |
|
8 | Na tuliwaangamiza walio kuwa na nguvu kushinda wao. Na mfano wa watu wa zamani umekwisha pita. |
|
9 | Na ukiwauliza: Nani aliye ziumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka watasema: Kaziumba Mwenye nguvu, Mjuzi, |
|
10 | Ambaye amekufanyieni ardhi kama tandiko, na akakufanyieni ndani yake njia mpate kuongoka. |
|
11 | Na ambaye ndiye aliye teremsha kutoka mbinguni maji kwa kiasi, na kwa hayo tukaifufua nchi iliyo kufa. Na namna hivi ndivyo mtakavyo tolewa. |
|
12 | Na ambaye ndiye aliye umba katika kila kitu jike na dume, na akakufanyieni marikebu na wanyama mnao wapanda. |
|
13 | Ili mkae vizuri migongoni mwao, kisha mkumbuke neema za Mola wenu Mlezi mnapokaa sawa sawa juu yao na mseme: Ametakasika aliye mfanya huyu atutumikie, na tusingeli weza kufanya haya wenyewe. |
|
14 | Na hakika sisi tutarudi kwa Mola wetu Mlezi. |
|
15 | Na wanamfanyia katika waja wake fungu. Kwa hakika mwanaadamu ni mtovu wa fadhila aliye dhaahiri. |
|
16 | Au amejichukulia watoto wanawake katika vile alivyo viumba, na akakuteulieni nyinyi watoto wanaume? |
|
17 | Na anapo bashiriwa mmoja wao kwa yale aliyo mpigia mfano Mwenyezi Mungu, uso wake husawijika na hujaa hasira. |
|
18 | Ati aliye lelewa katika mapambo, na katika mabishano hawezi kusema kwa bayana...? |
|
19 | Na wakawafanya Malaika, ambao ni waja wa Mwingi wa Rehema, ni wanawake! Kwani wameshuhudia kuumbwa kwao? Ushahidi wao utaandikwa na wao watahojiwa! |
|
20 | Nao husema: Angeli penda Mwingi wa Rehema tusingeli waabudu sisi. Hawana ujuzi wowote wa hayo! Hawana ila kusema uwongo tu! |
|
21 | Kwani tuliwapa Kitabu kabla ya hichi, na ikawa wao wanakishikilia hicho? |
|
22 | Bali wanasema: Hakika sisi tuliwakuta baba zetu wanashika dini makhsusi, basi na sisi tunaongoza nyayo zao. |
|
23 | Na kadhaalika hatukumtuma mwonyaji kwenye mji wowote ila watu wake walio deka kwa starehe walisema: Hakika sisi tuliwakuta baba zetu wanashika dini makhsusi, na sisi tunafuata nyayo zao. |
|
24 | Akasema (Mwonyaji): Hata nikikuleteeni yenye uwongofu bora kuliko mlio wakuta nao baba zenu? Wakasema: Sisi tunayakataa tu hayo mliyo tumwa. |
|
25 | Basi tukawalipizia. Angalia ulikuwaje mwisho wa walio kadhibisha! |
|
26 | Na pale Ibrahim alipo mwambia baba yake na kaumu yake: Hakika mimi ninajitenga mbali na hayo mnayo yaabudu, |
|
27 | Isipo kuwa yule aliye niumba, kwani Yeye ataniongoa. |
|
28 | Na akalifanya hili liwe neno lenye kubaki katika vizazi vyake ili warejee. |
|
29 | Bali tuliwastarehesha hawa na baba zao mpaka ikawafikia Haki na Mtume aliye bainisha. |
|
30 | Na ilipo wafikia Haki wakasema: Huu ni uchawi, na sisi hakika tunaukataa. |
|
31 | Na walisema: Kwa nini Qur'ani hii haikuteremshwa kwa mtu mkubwa katika miji miwili hii? |
|
32 | Kwani wao ndio wanao gawa rehema za Mola wako Mlezi? Sisi tumewagawanyia baina yao maisha yao katika uhai wa duniani, na tukawanyanyua baadhi yao juu ya wengine kwa daraja nyingi; kwa hivyo baadhi yao wanawafanya wenginewe wawatumikie. Na rehema za Mwenyezi Mungu ni bora kuliko hayo wanayo yakusanya. |
|
33 | Na lau isinge kuwa watu watakuwa kundi moja tungeli wajaalia wanao mkufuru Rahmani wana nyumba zao zina dari ya fedha, na ngazi zao pia wanazo pandia, |
|
34 | Na milango ya nyumba zao na vitanda wanavyo egemea juu yake, |
|
35 | Na mapambo. Lakini hayo si chochote ila ni starehe ya maisha ya dunia tu, na Akhera iliyoko kwa Mola wako Mlezi ni ya wenye kumchamngu. |
|
36 | Anaye yafanyia upofu maneno ya Rahmani tunamwekea Shet'ani kuwa ndiye rafiki yake. |
|
37 | Na hakika wao wanawazuilia Njia na wenyewe wanadhani kuwa wameongoka. |
|
38 | Hata atakapo tujia atasema: Laiti ungeli kuwako baina yangu na wewe kama umbali baina ya mashariki na magharibi. Rafiki mwovu mno wewe! |
|
39 | Na kwa kuwa mlidhulumu, haitakufaeni kitu leo kwamba nyinyi mnashirikiana katika adhabu. |
|
40 | Je! Unaweza kuwasikilizisha viziwi, au unaweza kuwaongoa vipofu na waliomo katika upotofu ulio wazi? |
|
41 | Na hata tukikuondoa, Sisi tutalipiza kisasi chetu kwao. |
|
42 | Au tutakuonyesha tulio waahidi. Nasi bila ya shaka tuna uweza juu yao. |
|
43 | Basi wewe yashike yaliyo funuliwa kwako. Hakika wewe uko kwenye Njia Iliyo Nyooka. |
|
44 | Na hakika haya ni ukumbusho kwako na kwa kaumu yako. Na mtakuja ulizwa. |
|
45 | Na waulize Mitume wetu tulio watuma kabla yako: Je! Tulifanya miungu mingine iabudiwe badala ya Rah'mani? |
|
46 | 46, Na bila ya shaka tulimtuma Musa kwa Ishara zetu ende kwa Firauni na waheshimiwa wake, na akasema: Hakika mimi ni Mtume wa Mola Mlezi wa walimwengu wote! |
|
47 | Lakini alipo wajia na Ishara zetu wakaingia kuzicheka. |
|
48 | Na hatukuwaonyesha Ishara yoyote ila hiyo ilikuwa kubwa zaidi kuliko nyenginewe. Na tukawakamata kwa adhabu ili warejee. |
|
49 | Na wakasema: Ewe mchawi! Tuombee kwa Mola wako Mlezi kwa ile ahadi aliyo kuahidi; hakika sisi tutakuwa wenye kuongoka. |
|
50 | Basi tulipo waondolea adhabu hiyo, mara wakaingia kuvunja ahadi. |
|
51 | Na Firauni alitangaza kwa watu wake, akisema: Enyi watu wangu! Kwani mimi sinao huu ufalme wa Misri, na hii mito inapita chini yangu? Je! Hamwoni? |
|
52 | Au mimi si bora kuliko huyu aliye mnyonge, wala hawezi kusema waziwazi? |
|
53 | Basi mbona hakuvikwa vikuku vya dhahabu, au hawakuja Malaika pamoja naye wakamwandama? |
|
54 | Basi aliwachezea watu wake, na wakamt'ii. Kwa hakika hao walikuwa watu wapotovu. |
|
55 | Walipo tukasirisha tuliwapatiliza tukawazamisha wote! |
|
56 | Kisha tukawafanya kuwa watangulizi na mfano kwa wa baadaye. |
|
57 | Na alipo pigiwa mfano Mwana wa Mariamu, watu wako waliupiga ukelele. |
|
58 | Wakasema: Miungu yetu kwani si bora kuliko huyu? Hawakukupigia mfano huo ila kwa ubishi tu. Bali hao ni watu wagomvi! |
|
59 | Hakuwa yeye (Isa) ila ni Mtumwa tuliye mneemesha na tukamfanya ni mfano kwa Wana wa Israili. |
|
60 | Na tungeli penda tungeli wafanyia miongoni mwenu Malaika katika ardhi wakifuatana. |
|
61 | Na kwa hakika yeye ni alama ya Saa ya Kiyama. Basi usiitilie shaka, na nifuateni. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka. |
|
62 | Wala asikuzuilieni Shet'ani. Hakika yeye ni adui yenu wa dhaahiri. |
|
63 | Na alipo kuja Isa na dalili zilizo wazi, alisema: Nimekujieni na hikima, na ili nikuelezeni baadhi ya yale mliyo khitalifiana. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na mnit'ii mimi. |
|
64 | Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu Mlezi, na ni Mola wenu Mlezi. Basi Muabuduni Yeye tu. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka. |
|
65 | Lakini makundi kwa makundi yao yalikhitalifiana wao kwa wao. Ole wao walio dhulumu kwa adhabu ya siku chungu. |
|
66 | Je! Nini wanangojea ila Saa iwajie kwa ghafla na wala wao hawatambui? |
|
67 | Siku hiyo marafiki watakuwa ni maadui, wao kwa wao, isipo kuwa wachamngu. |
|
68 | Enyi waja wangu! Hamtakuwa na khofu siku hiyo, wala hamtahuzunika. |
|
69 | Ambao waliziamini Ishara zangu na walikuwa Waislamu. |
|
70 | Ingieni Peponi, nyinyi na wake zenu; mtafurahishwa humo. |
|
71 | Watakuwa wanapitishiwa sahani za dhahabu na vikombe; na vitakuwamo ambavyo nafsi zinavipenda na macho yanavifurahia, na nyinyi mtakaa humo milele. |
|
72 | Na hiyo ni Pepo mliyo rithishwa kwa hayo mliyo kuwa mkiyafanya. |
|
73 | Mnayo humo matunda mengi mtakayo yala. |
|
74 | Kwa hakika wakosefu watakaa katika adhabu ya Jahannamu. |
|
75 | Hawatapumzishwa nayo na humo watakata tamaa. |
|
76 | Wala Sisi hatukuwadhulumu, bali wao ndio walio kuwa madhaalimu. |
|
77 | Nao watapiga kelele waseme: Ewe Malik! Na atufishe Mola wako Mlezi! Naye aseme: Hakika nyinyi mtakaa humo humo! |
|
78 | Kwa yakini tulikuleteeni Haki, lakini wengi katika nyinyi mlikuwa mnaichukia Haki. |
|
79 | Au waliweza kupitisha amri yao? Bali ni Sisi ndio tunao pitisha. |
|
80 | Au wanadhani kwamba hatusikii siri zao na minong'ono yao? Wapi! Na wajumbe wetu wapo karibu nao, wanayaandika. |
|
81 | Sema: Ingeli kuwa Rahmani ana mwana, basi mimi ningeli kuwa wa kwanza kumuabudu. |
|
82 | Ametakasika Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, Mola Mlezi wa A'rshi, na hayo wanayo msifia. |
|
83 | Basi waache wapige porojo wakicheza mpaka wakutwe na hiyo siku yao waliyo ahidiwa. |
|
84 | Na Yeye ndiye Mungu mbinguni, na ndiye Mungu katika ardhi. Naye ndiye Mwenye hikima, Mwenye ujuzi. |
|
85 | Na ametukuka Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi na viliomo ndani yake. Na uko kwake ujuzi wa Saa ya Kiyama, na kwake Yeye mtarudishwa. |
|
86 | Wala hao mnao waomba badala yake Yeye hawana uweza wa kumwombea mtu, isipo kuwa anaye shuhudia kwa haki, na wao wanajua. |
|
87 | Na ukiwauliza ni nani aliye waumba? Bila ya shaka watasema: Mwenyezi Mungu! Basi ni wapi wanako geuziwa? |
|
88 | Na usemi wake (Mtume) ni: Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika hawa ni watu wasio amini. |
|
89 | Basi wasamehe, na uwambie maneno ya salama. Watakuja jua. |
|